ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, August 20, 2017

MICHUANO YA "IKUNGI ELIMU CUP 2017" YAZINDULIWA KWA KISHINDO WILAYANI IKUNGI

Mgeni rasmi, Katibu Tawala mkoa wa Singida Dkt.Angeline Lutambi, akizungumza kwenye ufunguzi wa michuano ya soka ya "Ikungi Elimu Cup 2017" kwa niaba ya Mkuu wa mkoa huo Dkt.Rehema Nchimbi.

Michuano hiyo ilizinduliwa jana kwenye uwanja wa shule ya sekondari Ikungi, lengo ikiwa ni kuhamasisha wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa elimu kusaidia kutatua baadhi ya changamoto za elimu wilayani Ikungi ikiwemo ujenzi wa madarasa, maabara, nyumba za waalimu pamoja na vyoo.

Michuano ya soka ya “Ikungi Elimu Cup 2017” imezinduliwa kwa kishindo katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida baada ya mamia ya wakazi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo.

Michuano hiyo iliyoandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi na kuendeshwa na Chama cha Soka wilayani Ikungi, ilizinduliwa jana Agosti 19,2017 katika uwanja wa shule ya sekondari Ikungi huku ikitarajiwa kushirikisha timu 69 wilayani humo.

Mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala mkoa wa Singida Dkt.Angeline Lutambi, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida ambaye alipongeza wazo la kuanzishwa kwa michuano hiyo inayolenga kuhamasisha wananchi pamoja wadau mbalimbali ndani na nje ya wilaya ya Ikungi ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kutatua changamoto za elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa, maabara, vyoo pamoja na nyumba za waalimu.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mhe.Miraji Mtaturu ambaye ni mlezi wa mfuko wa elimu Ikungi, alisema michuano hiyo itasaidia upatikanaji wa shilingi bilioni tatu kupitia mfuko wa elimu Ikungi katika kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya kusaidia utatuzi wa kero za elimu wilayani huo.


Uzinduzi wa michuano hiyo, ulikwenda sambamba na uzinduzi wa zoezi la ufyatuaji wa matofali kwa ajili ya ujenzi wa maabara uliokwama tangu mwaka 2009 katika shule ya sekondari Ikungi hii ikiwa ni uzinduzi rasmi wa zoezi kama hilo kwenye kata zote wilayani Ikungi ambapo kila Kata imepewa jukumu la kufyatua matofali elfu kumi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na nyumba za waalimu.

Katika zoezi hilo, walijitokeza wadau pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani, wenyeviti wa halmashauri, jeshi la polisi, Tanesco na wanachi ambao walimuunga mkono Mkuu wa wilaya ya Ikungi, Mhe.Mtaturu aliyekabidhi mifuko 100 ya simenti na wao wakachangia fedha taslimu zaidi ya shilingi 800,000 na ahadi zaidi ya shilingi 1,900,000, ahadi za simenti mifuko 194 na mchanga wa moramu malori matano kutoka kwa mdau wa maendeleo wilayani Ikungi Hussein Sungita.

Aidha mgeni rasmi aliwakabidhi shilingi laki moja kila mmoja, jumla ya wanafunzi 16 wa kidato cha sita shule ya sekondari Ikungi waliopata daraja la kwanza kwenye mtihani wao ikiwa ni ahadi ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu aliyoitoa wakati wa mahafali ya wanafunzi hao huku akiwaahidi walimu shilingi milioni moja kwa kila wanafunzi 10 wenye madaraja ya kwanza.

Nazo timu 69 zinazoshiriki michuano hiyo ya “Ikungi Elimu Cup 2017” zilipokea vifaa vya michezo ikiwemo jezi na mipira kwa ajili ya michuano hiyo ambapo jana zilipigwa mechi mbili za kirafiki, ya kwanza ikiwa ni kati ya madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Singida dhidi ya madiwani wa halmashauri ya Ikungi ambapo mchezo huo ulimalizika kwa sare tasa.

Mchezo wa pili ulikuwa kati ya Ikungi United dhidi ya Puma ukimalizika kwa puma kuwashangaza Ikungi waliokuwa wanaongoza kwa bao mbili hadi kipindi cha kwanza, baada ya kusawazisha na kujipatia bao la ushindi katika kipindi cha pili na hivyo matokeo kuwa Puma 3-2 Ikungi.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe.Miraji Mtaturu akizungumza kwenye uzinduzi huo
Mgeni rasmi akishiriki shughuli ya ufyatuaji tofali kwa ajili ya ujenzi wa maabara katika shule ya sekondari Ikungi ikiwa ni uzinduzi wa shughuli kama hiyo katika Kata zote wilayani Ikungi ambazo zitashiriki kufyatua tofali elfu kumi kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa madarasa na nyumba za waalimu.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi, Mhe. Miraji Mtaturu akishiriki zoezi la ufyatuaji matofali
Matofali kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya shule ya sekondari Ikungi ambayo ujenzi wake ulikwama tangu mwaka 2009
Mwenyekiti wa wa halmashauri ya Ikungi akishiriki zoezi hilo
Zoezi la ufyatuaji matofali ukiendelea ambapo viongozi mbalimbali walishiriki
Katibu wa CCM mkoa wa Singida akishiriki zoezi hilo
Mkuu wa wilaya ya Ikungi (kulia) akipokea michango ya papo kwa papo kutoka kwa viongozi mbalimbali waliojitokeza kumuunga mkono katika kusaidia utatuzi wa changamoto za elimu wilayani humo kupitia mfuko wa elimu Ikungi
Mkuu wa wilaya ya Ikungi (wa pili kushoto) Miraji Mtaturu akikabidhi mifuko 100 ya simenti aliyoahidi kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa maabara ya shule ya sekondari Ikungi ambapo wadau wengine walimuunga mkono kwa kuchangia mifumo mingine 194 na hivyo jumla ikapatikana mifuko 294
Msingi wa jengo la maabara katika shule ya sekondari Ikungi ambao ujenzi wake umekwama tangu mwaka 2009 huku mbunge wa jimbo la Singida Mashariki, Mhe.Tundu Lissu akilalamikiwa kukwamisha ujenzi huo baada ya kuwazuia wananchi kutoshiriki kwenye michango mbalimbali ya maendeleo
Mgeni rasmi akiwakabidhi wanafunzi 16 wa kidato cha sita waliopata daraja la kwanza katika shule ya sekondari Ikungi shilingi laki moja, ikiwa ni ahadi ya mkuu wa wilaya ya Ikungi aliyoitoa kwa kila mwanafunzi atakayepata daraja hilo. Wanafunzi 16 walipata daraja la kwanza kwenye mtihani wao wa kidato cha sita. Pia waalimu waliahidiwa shilingi milioni moja kwa kila wanafunzi 10 wenye daraja la kwanza.
Mwanafunzi wa kidato cha sita shule ya sekondari Ikungi akipokea shilingi laki moja baada ya kupata daraja la kwanza kwenye mtihani wake
Timu zote 69 zinazoshiriki michuano ya Ikungi Elimu Cup zilipatiwa vifaa vya michezo ikiwemo jezi na mipira miwili
Timu shiriki za Ikungi Elimu Cup zikipatiwa jezi na mipira kwa ajili ya ligi
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi (kulia) na mwenyekiti wa halmashauri ya Ikungi (kushoto) wakiingia uwanjani kwenye mchezo wa kirafiki na timu ya Manispaa ya Singida
Mkuu wa wilaya ya Ikungi akipiga penati kama ishara ya ufunguzi wa michuano ya Ikungi Elimu Cup 2017
Go Goo Goooooooo!
Mgeni rasmi akiwa na kikosi cha timu ya madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Singida kilichocheza na timu ya madiwani wa Halmashauri ya Ikungi kikiongozwa na Mkuu wa wilaya ya Ikungi na matokeo yakawa ni suluhu ya bila kufungana
Mgeni rasmi akiwa kwenye picha ya pamoja na kikosi cha madiwani wa halmashauri ya Ikungi kilichocheza na kikosi cha madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Singida na matokeo yalikuwa ni suluhu ya bila kufungana
Baadaye kuliwa na mchezo kati ya timu zinazoshiriki ligi ya Ikungi Elimu Cup ambapo Ikungi United walicheza na Puma na Ikungi wakakubali kufungwa bao 3-2.
Ikungi United na Puma zikisalimia kabla ya kuanza kuchuana kwenye mchezo wa kirafiki kuelekea kwenye ligi ya Ikungi Elimu Cup 2017. Matoke yalikuwa ni Puma 3-2 Ikungi
Katibu wa CCM ikungi akifurahia ngoma ya asili iliyotumbuizwa na kikundi cha Nyota Njema
Kamanda wa polisi mkoani Singida, Debora Magirigimba aliwataka vijana kujikita kwenye michezo na kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya huku pia akiwaonya wanaowapa mimba wanafunzi na kwamba atakaebainika kujihusisha kimapenzi na mwanafunzi atachukuliwa hatua kali za kisheria
Ikungi Elimu Cup-Changia, Boresha Elimu Ikungi
BMG Habari

No comments: