ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 26, 2017

DC BARIADI AISWEKA RUMANDE KAMATI YA SHULE KWA MATUMIZI MABAYA YA SHILINGI MILIONI 4.8

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kuwaweka rumande wajumbe watano wa Kamati ya Ujenzi ya Shule ya Msingi Bariadi, baada ya kudaiwa kutumia vibaya fedha za ujenzi wa matundu 14 ya vyoo vya shule hiyo.
Kamati hiyo inadaiwa kutumia kiasi cha Sh 4.8 Milioni ambazo zilichangwa na wananchi kwa ajili ya ujenzi huo ili kupunguza uhaba wa matundu ya vyoo uliokuwa unaikabili shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 1,373.
Akizungumza shuleni hapo leo Jumanne, Kiswaga aliwataja waliokamatwa kuwa ni mwenyekiti wa kamati hiyo, Mlela Hosea, makamu wake Lucas Gervas na wajumbe Kenedy Machume, Wodya Husein na Suzan Ezekiel.
Kiswaga aliwaonya wote wenye tabia ya kugusa fedha zinatokana na michango ya wananchi kuwa Serikali yake itawashughulikia ipasavyo kwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani na kuwataka wananchi waendelee kuchangia fedha kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Akizungumzia suala hilo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bariadi, Mayila Ndalahwa amesema dalili za wajumbe hao kufuja fedha zilizochangwa na wananchi zilianza kuonekana mapema baada ya kumfukuza fundi aliyekuwa ameidhinishwa na mkutano mkuu wa wazazi.
“Kila mzazi alichangia Sh7,600 ili kufanikisha ujenzi huo na kamati hiyo ilitokana na wazazi wenyewe, ilionekana walianza kununua vifaa hewa kwa sababu walikuwa wakichukua fedha nyingi lakini wanaleta vifaa vichache,” amesema Ndalahwa

Chanzo: Mwananchi

No comments: