ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 6, 2017

MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AZINDUA MAKAO MAKUU YA KAMISHENI YA KISWAHILI YA AFRIKA MASHARIKI

04 Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akiwaonyesha wajumbe walioshiriki Kongamano la kwanza la Kimataifa la Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki mpango mkakati wa miaka mitano wa Kamisheni hiyo (kulia) Mtendaji Mkuu wa Kamisheni Prof. Kenneth Simala na (kushoto) Rais Mstaafu wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi.

Maryam Kidiko na Mwashungi Tahir-Maelezo Zanzibar.
KUANDALIWA kwa kongamano la kwanza la Kimataifa la Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ni miongoni mwa juhudi za kuendeleza lugha ya Kiswahili katika ukanda huo na Duniani kwa jumla.
 Hayo ameyasema Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki huko katika ukumbi wa  Hoteli ya Golden Tulip iliopo Malindi Mjini Zanzibar.
 Alisema kongamano hilo lililowashirikisha wataalamu wa lugha ya Kiswahili wa nchi wananchama wa Afrika Mashariki  lina umuhimu mkubwa katika historia ya maendeleo ya Kiswahili duniani pamoja na kupanga mikutano na kubadilishana utalaamu .
  Hivyo Alieleza kuwa ni muhimu kwa kamisheni kusimamia kwa makini hadhi ya Kiswahili kama lugha ya mawasiliano ikitambuwa kwamba ukanda wa Afrika Mashariki ni sehemu ya Dunia yenye lugha tofauti.
 Samia alisema uratibu na uendelezaji wa Maendeleo na matumizi ya Kiswahili utaimarisha mchakato na utengamano wa Jumuiya kwa maendeleo endelevu. “Utengamano wa Jumuiya sio tukio bali ni mchakato ambao unapaswa kuendeshwa na watu wenye kuelewa vizuri matumizi endelevu ya Kiswahili “Alisema Makamo wa Rais.
 Hata hivyo alielezea kuwa mafanikio kamili yanategemea mkabala wa mawasiliano na ushiriki wa raia wote katika maendeleo endelevu ya Jumuiya . Alisema Kiswahili ni kiungo muhimu kati ya wana Afrika Mashariki katika kujenga utambuzi na kubaini changamoto pamoja na fursa zinazofungamana na maendeleo.
 Alitaka kongamano hilo kuonyesha namna ambavyo Kiswahili kinaweza kufanikisha utangamano na malengo  ya kuimarisha maendeleo ya nchi wanachama Afrika Mashariki.  Waziri Samia alionyesha kkufurahishwa kwake na nchi wanachama kutenga bajeti kila mwaka kwa lengo la kuimarisha na kuendeleza shughuli za Kamisheni hiyo.
Nae Waziri wa Habari  Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe alisema baadhi ya Nchi za ukanda wa Afrika Mashariki ambazo zilikuwa nyuma katika kutumia lugha ya Kiswahili wamepiga hatua na kimeweza kusaidia katika kuharakisha maendeleo yao.
  Aliitaka Kamisheni hiyo  kushirikiana na Wadau mbali mbali ili iweze kuleta maendeleo kupitia  lugha ya Kiswahili.
 Kwa upande wa Waziri wa Habari Utalii , Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma alisema Serilkali ya Zanzibar  inathamini kuwepo Makao Makuu ya Kamisheni  Zanzibar na ameahidi itaendelea kuunga mkono  kutokana na umuhimu wa lugha hiyo.
 Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Profesa Kenneth Simala alisema Kamisheni itafanya juhudi ya kuziunganisha nchi wanachama na asasi za kiraia  kukikuza Kiswahili.
 Sambamba na hayo alisema Zanzibar imeweza kutowa mchango mkubwa katika Nchi za Afrika Mashariki  kupitia lugha ya Kiswahili katika kukuza lugha hiyo.
 Kauli mbiu ya Kongamano hilo la siku mbili ni ‘KULETA MABADILIKO KATIKA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI KUPITIA KISWAHILI.

No comments: