Advertisements

Saturday, September 16, 2017

Meya Chadema akabidhi barua Ikulu

By Daniel Mjema na Asna Kaniki, Mwananchi Mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya (Chadema), amekabidhi barua ofisi ya Rais Ikulu, akiomba kuonana na Rais John Magufuli kwa niaba ya baraza lake la madiwani.

Habari ambazo zimepatikana na kuthibitishwa na meya huyo, zimesema yapo mambo mawili makubwa ambayo anaomba kuonana na Rais ili amweleze kwa kina likiwamo suala la upanuzi mji wa Moshi.

Upanuzi wa mji huo kutoka kilometa za mraba 58 za sasa hadi kilometa za mraba 142, ungeufanya mji huo kukamilisha vigezo vya kuwa Jiji, ndoto ambayo ilikuwapo tangu mwaka 2012.

Mchakato huo umesitishwa na Rais Magufuli Aprili 30,2017 alipokutana na viongozi wa dini, ambapo mchungaji mmoja alidai katika kikao hicho kuwa Manispaa ya Moshi inataka kuwapora ardhi yao.

Wakati Rais Magufuli akisitisha mchakato huo, tayari Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willian Lukuvi, alikuwa amesaini sheria ya kuviingiza vitongoji 40 katika Manispaa ya Moshi.

Vitongoji hivyo vipo katika mamlaka ya Halmashauri ya wizaya za Hai na Moshi na mchakato wa kuviingiza vijiji hivyo katika mamlaka ya Manispaa ya Moshi, ulipitia hatua zote za kisheria.

Kuingizwa kwa vitongoji hivyo 40 kulifanya mji huo kukidhi kigezo cha kuwa Jiji ambapo Lukuvi kupitia tangazo la Serikali namba 219 la Julai 15 mwaka huu, aliviingiza vitongoji hivyo Moshi mjini.

Mboya alipotafutwa gazeti hili jana alithibitisha kusafiri hadi Jijini Ijumaa iliyopita na kwenda hadi Ikulu na kupokelewa vizuri ambapo barua yake ilipokelewa na kuingizwa ndani Ikulu.

“Kwa kweli nilipokelewa vizuri sana na barua yetu ikapokelewa na kuandikishwa kisha ikaingizwa ndani. Waliniambia nitapigiwa simu sasa sijajua ni lini ndio nasubiria,”amesema Mboya.

“Sababu kubwa za kuomba kumuona Rais ni mbili. Moja ni upanuzi wa mji wetu. Tunataka tumpe ripoti kamili ya mchakato ulivyoenda. Tunaon Rais hakupewa taarifa kamili alipositisha,”amesema.

“Zuio la Rais limekuja wakati tayari tulikuwa tumesaini mkataba wa Sh700 milioni na kampuni ambayo ingeandaa mpango wa Jiji wa miaka 20 na walikuwa wapo eneo la mradi,”amesisitiza.

Mboya alisema, jambo la pili lililowasukuma kuomba kuonana na Rais, ni kumuomba awasaidie waweze kupata kibali cha ujenzi wa stendi mpya na ya kisasa katika eneo la Ngangamfumuni.

Kwa mujibu wa Mboya, wamelazimika kumuomba Rais kwa vile wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), iko chini yake na hawaelewi kwanini wanazungushwa kupewa kibali.

Wiki iliyopita, Mbunge wa Moshi mjini (Chadema), Jaffar Michael naye alijitokeza mbele ya wanahabari akisema suala la kukwama kwa mradi huo, ataliwasilisha kwa Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, mradi huo mkubwa wa kiuchumi unaotakiwa kujengwa eneo laNgangamfumuni kwa gharama ya Sh20.7 bilioni, umepitia hatua zote za kikanuni na kisheria.

“Ninamsihi Rais wetu atoe kibali cha ujenzi maana Tamisemi iko chini yake. Tuna mashaka huenda mheshimiwa Rais hajaelezwa vizuri juu ya mradi huu wa wananchi wa Moshi,”amesema.

Mbunge huyo alisema makubaliano yaliyopo ni kuwa Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB), ndio ambayo ilikuwa ihusike kwenye michoro, kujenga na kuuendesha mradi kwa miaka 15.

“Baada ya miaka 15 TIB wangerudisha mradi kwa Halmashauri baada ya kurejesha mkopo wao na riba. Leo tunaambiwa tuzungumze na Lapf (mfuko wa pensheni) ambao hawana mpango nao,”amesema.

Hivi karibuni, aliyekuwa waziri wa Tamisemi, George Simbachawene, alikanusha yeye kuwa kikwazo cha kuanza kwa mradi akisema lazima kwanza ajiridhishe kama una manufaa ya kichumi.

“Wala mimi sio kwamba nakataa lakini na mimi ili niweze kuruhusu nahitaji ushauri wa kitaalamu na kujiridhisha sasa wataalamu wangu wananiambia stendi Moshi haitalipa,”amesema Simbachawene.

“Haitalipa kwa sababu magari mengi destination (kituo) ni Arusha na wanapofanya hiyo mikopo yao wanaingia kwa miaka mingi kwa hiyo Halmashauri italipa kwa muda mrefu,”amesisitiza.

Simbachawene alisema kabla Halmashauri haijaingizwa katika deni hilo ni lazima kujiridhisha juu ya uhalisia wa mradi wenyewe na uwezo wa kupata mapato na kulipa mkopo kwa muda wa mkataba.

“Si vyema kuiingiza Halmashauri kwenye deni halafu biashara ikashindwa kujilipa halafu wakaanza kuchukua vyanzo vingine kulipa deni. Hiyo haiwezi ikakubalika hata kidogo,”alisisitiza Waziri.

Kumekuwepo na mvutano mkubwa kati ya Serikali na Meya na Mbunge juu ya mradi huo, huku viongozi hao wa kisiasa wakinusa kile kinachodaiwa kinachangiwa na Baraza kuwa upinzani.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Rais Ikulu Gerson Msigwa alipoulizwa na gazeti hili kuhusu barua hiyo amesema “mawasiliano ya barua ni kati ya aliyeandika na aliyeandikiwa sasa nyie gazeti la mwanchi mnaingiaje? nyie ni wadukuzi?,” alihoji Msigwa.

“Ngoja niwaulize kitu nyie watu wa gazeti la mwanachi hivi barua zote zinazoenda kwa Rais mnataka kuulizia hivi nyie mna ajenda gani?,” amehoji.

“Juzi pia mwenzako kaulizia kuhusu barua kwa Rais, inamaana nyie mwananchi mnachanel ya kufuatilia barua zinazoingia katika ofisi ya mawasiliano ya Rais” amesema.

“Kuna mambo yanakera mimi nimwandishi mwenzako, huwezi kufuatilia barua zinazoingia kwa Rais hii ni nchi ya namna gani?,” amehoji.

“Kama mnataka hiyo kazi ya kufuatilia barua za wanaoandika nyie endeleeni, nyie kila siku nasikiliza simu zenu tu si muwaambie hao watu kama wameandika barua wasubirie majibu walikoandika”amesema

No comments: