ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 31, 2017

DKT NCHIMBI ATOA MWEZI MMOJA KWA HALMASHAURI YA IRAMBA KUJENGA VYOO KATIKA MNADA WA MALENDI

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na wananchi waliokuwa wamepanga foleni kulipa ushuru katika mnada wa Malendi Wilayani Iramba.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akikagua mnada wa Malendi Wilayani Iramba ambapo amemuagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhakikisha anajenga vyoo na kufikisha huduma za maji ndani ya mwezi mmoja.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Malendi na maeneo ya jirani waliokuwa katika mnada huo wakinyoosha mikono kumsalimia Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi alipowatembelea mnadani hapo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amempa mwezi mmoja Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Iramba, kujenga vyoo bora katika Mnada uliopo Kijiji cha Malendi, kata ya Mgongo Wilayani humo.

Dkt Nchimbi ametoa agizo hilo mara baada ya kutembelea mnada huo ambapo wananchi wamelalamika kukosa huduma za vyoo na maji kwa kipindi kirefu huku halmashauri ikikusanya ushuru bila kuwaboreshea miundombinu ya mnada huo.

“Mkurugenzi nakupa mwezi mmoja hapa kuwe na vyoo bora vikiwa na matundu sita kwa ajili ya wananchi hawa pamoja na huduma za maji, kipindi cha mvua kinaanza, lazma muwajali wananchi hawa kwakuwa kipindupindu kinaweza kulipuka hapa”, ameeleza Dkt Nchimbi.

Ameongeza kuwa kwakuwa hakuna vyoo wananchi watajisaidia maeneo ya jirani na mnada na mvua zikianza zitatiririsha uchafu huo katika eneo la mnada na makazi ya wanakijiji cha Malendi na hivyo kusababisha mlipuko wamagonjwa hasa Kipindupindu.

Dkt Nchimbi amesema Mkurugenzi huyo ajenge vyoo vyenye matundu sita pamoja na kuvuta huduma za maji kwakuwa maji husaidia usafi wa eneo hilo na kupunguza uwezekano wa magonjwa hayo.

“Halmashauri mna jukumu la kuhakikisha mnada huu una miundombinu yote hasa ya maji na vyoo kwakuwa mnakusanya ushuru pia kumbukeni kuhakikisha huduma zinapatikana vizuri mnadani hapa”, ameelekeza Dkt Nchimbi.

Aidha amewataka Wakurugenzi wa halmashauri za Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na idara za usafi wa mazingira na Wakala wa barabara vijijini (TARURA) wanahakiki njia na mitaro ya kupitisha maji ili mvua zisilete maafa pamoja na kuhakiki mabwawa ili baada ya mvua kuisha waweze kuvuna maji ya kutosha.

Dkt Nchimbi ameeleza kuwa mvua za msimu uliopita zilileta maafa ya kipindupindu hivyo hatarajii kwa mvua za msimu huu kuleta tena magonjwa kwakuwa wakurugenzi wametahadharishwa mapema uwepo wa mvua za wastani na juu ya wastani.

Ameongeza kwa kuwashauri wananchi kuimarisha makazi yao ili yaweze kuhimili mvua hizo pamoja na kujenga vyoo bora ili wasipate magonjwa hasa kipindupindu.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iramba Marietha Kasongo amesema amelipokea agizo hilo na kuongeza kuwa mwezi mmoja unatosha kujenga vyoo hivyo na kufikisha huduma za maji mnadani hapo.

Amesema halmashauri ilikuwa na mpango wa kujenga vyoo na kuvuta maji mnadani hapo hivyo agizo la Mkuu wa Mkoa limewaamsha ili waweze kutekeleza mipango yao kwa haraka zaidi.

Awali Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini imetangaza kuwa Mkoa wa Singida unatarajiwa kupata mvua za wastani na juu ya wastani, aidha wastani wa mvua kwa Mkoa wa Singida ulikuwa ni Milimita 500 mpaka 850.

No comments: