ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, October 29, 2017

Kamati ya PAC yaibana NSSF mradi wa Eco Village

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeliagiza Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuiondoa Kampuni ya Udalali ya Yono kwenye mradi wa Dege Eco Village ambayo hivi karibuni ilitangaza kupiga mnada mali za mradi huo.

Yono kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ilitangaza kupiga mnada mali hizo ili kufidia deni la kodi ya Sh45 bilioni lililokuwa akidaiwa mkandarasi wa mradi huo, Kampuni ya Ujenzi ya Mutluhan kutoka nchini Uturuki.

Mradi huo ulikuwa gumzo nchini baada ya ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kubaini uwapo wa ubadhirifu.

NSSF waliingia ubia na Kampuni Binafsi ya Azimio Housing Estate Limited, lakini baadaye ikaibuka shaka ya upotevu wa zaidi ya Sh270 bilioni.

Jana, mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka alitoa agizo hilo baada ya kamati kupitia hesabu za NSSF za mwaka wa fedha 2015/16.

“NSSF ikanushe tangazo mara moja la kuuza mradi wa Dege ambalo lilitolewa na Kampuni ya Udalali ya Yono. NSSF iifahamishe TRA kuwa ule mradi si mali ya mkandarasi, hivyo wawaondoe Yono kwenye eneo la mradi,” alisema Kaboyoka.

Kamati pia imeitaka Bodi ya NSSF kuchukua hatua za dharura kwa kushirikiana na mkandarasi aliye eneo la mradi ili kuokoa mali zilizopo.

“Sasa ni juu yenu, mtaamua mumrejeshe mkandarasi au mnatumia njia gani ili mali iliyopo pale isizidi kuharibika na kuharibiwa,” alisema Kaboyoka.

Pia, aliitaka Bodi ya NSSF kukamilisha mapitio ya mkataba kati yake na mbia kwa masilahi mapana ya Taifa na taarifa ya utekelezaji ipelekwe kwa Spika wa Bunge kabla ya Novemba 15.

Awali, akichangia hoja hiyo, mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alisema Yono ilitangaza katika mitandao kuwa itapiga mnada mali zilizoko katika mradi huo ili kufidia kodi anayodaiwa mkandarasi.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema baada ya kusikia tangazo hilo waliwasiliana na Yono na walisitisha.

Hata hivyo, wabunge waliwabana viongozi hao wakiwahoji ni kwa nini hawakukanusha tangazo hilo baada ya kubaini halina ukweli.

Makamu mwenyekiti wa kamati ya PAC, Aeshi Hillal aliitaka NSSF kuhakikisha mradi huo unafanya kazi hata kama wanataka kuongeza mbia mwingine.

“Hatuwezi kutafuta mbia kwa sasa wakati mradi uko katika hatua hii. Hakuna mtu atakayeweza kukubali.

“Pia, kuna gharama ambazo zinaendelea kuwapo pale, fanyeni mradi huu hata kama utaanza kwa awamu kuliko kuendelea hivi na fedha zinaendelea kutumika na vifaa vinaibwa,” alisema Hillal.

Mwenyekiti wa Bodi ya NSSF, Profesa Samwel Wangwe alisema wamepokea maagizo hayo na watakwenda kuyafanyia kazi kama kamati ilivyoshauriwa.

No comments: