MWANAMUZIKI Rehema Chalamila ‘Ray C’ amesema hatasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanamuziki wanaoimba nyimbo zake bila makubaliano
Nyota huyo ambaye kwa sasa yupo nje ya nchi ameimbia Mwananchi kuwa hawezi kuvumilia vitendo hivyo kwasababu vinalenga kumuharibia biashara yake ya muziki ambayo ndio maisha yake.
Amesema, “Muziki ni biashara huwezi ukalipwa pesa nyingi halafu ukapanda jukwaani ukaimba nyimbo za msanii mwingine bila makubaliano. Huu ni ufinyu wa ubunifu,”
Kauli hiyo ya Ray C imekuja siku moja baada ya kuandika kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa hakufurahishwa na kitendo cha Nandy kuimba wimbo wake bila ridhaa yake.
Aliandika, “Jamani hii tabia siyo nzuri. Kama mnaona umuhimu wa sauti yangu kwenye show zenu muwe mnaniita basi. Sina saratani ya koo ya kushindwa kuziimba hizo nyimbo! Nandy hii ni mara ya mwisho ukipanda tena fanya kazi zako.
Hii ni mara ya pili ujue! Mashabiki zangu hamuwatendei haki, maana hatatukigongana muda mwingine hata salamu hamnipi kwa hiyo sitaki mazoea,”
Haikupita muda mrefu Nandy naye akajibu, “Dada angu Ray C, mimi ni mmoja wa wasanii wanaokukubali ulikuwa miongoni mwa watu mliotufungulia njia ya muziki wetu ulipo. Sitaacha kukuheshimu na kukubali, siamini kukusifia na kukuenzi ni lazima uwe umekufa’’.
“Nafanya jambo hili zuri kwa moyo wangu mzuri kama ulivyomuenzi mama Mwanahela kwa nyimbo zake. Heshima yangu kimuziki kwako itabaki siku zote kama nilivyoimba nyimbo za wengine,”.
Hata hivyo Ray C amesema hana ukaribu wala mazoea na Nandy kiasi cha kuamua kuimba nyimbo zake bila makubaliano.
“Sikutaarifiwa na wala sikushirikishwa, mimi nilishawahi kurekodi cover za Mwanahela lakini nilimfuata nikamlipa na akanipa baraka zake. Sheria za hatimiliki zinajulikana ndiyo maana tuna Cosota,”
No comments:
Post a Comment