ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 30, 2017

MAKAMU WA RAIS AZINDUA SERA YA TAIFA YA HUDUMA NDOGO YA FEDHA MJINI DODOMA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akionyesha kitabu cha sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017 pamoja na Mkakati wa Utekelezaji mara baada ya kukizindua kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Mkurugenzi Mtendaji wa FSDT Bw. Sosthenes Kewe.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa uzinduzi wa sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017 pamoja na Mkakati wa Utekelezaji uliofanyika kwenye ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais) 



MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan leo amezindua sera ya Taifa ya huduma ndogo za fedha ya mwaka 2017 pamoja na mkakati wa utekelezaji wa mwaka 2017/2018 hadi 2027/2028 huku akizitaka taasisi za fedha nchini kuangalia kwa kina suala la riba linalokuwepo kwenye mikopo kwa kuwa limekuwa likiwaumiza wananchi wa hali ya chini.

Akizindua sera hiyo mjini Dodoma alisema lengo la kutoa mikopo hiyo ni kuwainua watanzania kiuchumi na sio kuwarudisha nyuma.

"Ndugu zangu jambo kubwa linalorudisha nyuma ni riba,inaturudisha nyuma sana hasa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo,kwa mtindo huu uliopo wa riba kubwa tunakuwa hatupigani na umaskini bali tunapigana na wamaskini au mafukara,"alisema Makamu wa Rais.

Alisema uwepo wa sera hiyo ni ushahidi tosha wa dhamira ya dhati ya serikali katika kuimarisha huduma za kifedha nchini na kuwa bora zaidi na kushauri kufanyika kwa tathmini ya utekelezaji wa sera iliyopita.

Aliiagiza ofisi ya rais tawala za mikoa na serikali za mitaa(TAMISEMI)kuhakikisha kuwa halmashauri zote nchini zinatenga asilimia 10 ipasavyo,halmashauri zitenge maeneo rasmi ya kuwawezesha wajasiriamali kuweza kujiajiri.

"Maeneo hayo maalum yawepo kwa ajili ya wajasiriamali na wafanya biashara wadogo wadogo ili wasiweze kusumbuliwa na mgambo lakini pia halmashauri iwasaidie wananchi kuuda vikundi vya fedha na Saccos ili kuwa katika mifumo rasmi ya kibenki"alisema Makamu wa Rais

Makamu wa Rais alisema dhamira ya Serikali ni kuinua uchumi wa wananchi wa kipato cha chini na Uzinduzi wa Sera hii ni mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya CCM inayosisitiza kupambana na umaskini hasa kwa kuwekea mkazo kwenye urasimishaji wa biashara na kuwapatia wafanyabiashara wadogo maeneo rasmi ya kufanyia biashara  ikiwa ni pamoja na kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu.

Makamu wa Rais alisisitiza elimu ya masuala ya fedha na ujasiriamali itolewe kwa wingi kwa wananchi wa kipato cha chini na wanaofanya kazi katika mifumo isiyo rasmi ikiwa pamoja na elimu inayoendana na mazingira ya sasa na mabadiliko ya kiteknolojia ambapo matumizi ya simu katika masula ya fedha yameenea nchini

Mwisho Makamu wa Rais alihitimisha kwa kusema Uzinduzi wa Sera hii Mpya na yale yaliyomo katika sera hii ni ushahidi tosha wa dhamira ya Serikali  na ya wenzetu wote tulioshirikiana nao katika kutayarisha sera hii kuona huduma za kifedha nchini zinazidi kuimarika na kuwa bora zaidi.

No comments: