ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, October 8, 2017

MASAUNI ATAKA MKANDARASI ACHUKULIWE HATUA KWA KUUTELEKEZA MRADI WA MABILIONI GEREZA IDETE

Image result for hamad masauni
Na Felix Mwagara (MOHA)
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amelitaka Jeshi la Magereza kumchukulia hatua kali Mkandarasi wa mradi mkubwa wa umwagiliaji wa Gereza la Kilimo Idete wilayani Kilombero endapo atabainika alifanya makosa kwa  kuutelekeza mradi huo.

Mradi huo ambao ungesaidia kuendeleza kilimo cha mpunga na mahindi kwa zaidi ya ekari 1000, unathamani ya zaidi ya Bilioni 2.5 ambapo ulianza kujengwa mwaka 2013 mara bada ya Serikali kumpa Mkandarasi huyo wa Kampuni ya Tanzania Building Works ya Dar es Salaam, zaidi ya Bilioni 1 ili kuufanikisha mradi huo katika hatua ya awali.   

Akizungumza mara baada ya kuukagua mradi huo uliopo Idete mkoani Morogoro, Masauni alisema Serikali ya Awamu ya Tano haitakubali uzembe huo kwa fedha za Serikali kuchezewa huku mradi huo haujakamilika.

Masauni alilitaka Jeshi la Magereza kuhakikisha Mkandarasi huyo ambaye fedha alizopewa haziendani na ukubwa wa kazi alizozifanya, achunguzwe haraka iwezekanavyo na endapo ikibainika amefanya makosa hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.


“Fedha ni nyingi alizopewa, zaidi ya bilioni moja za Serikali zimetolewa, na ukiangalia ukubwa wa  kazi aliyoifanya haiendani na thamani ya fedha hizo, hivyo hatuwezi kuvumilia na kuona fedha za Serikali zikichezewa, nahitaji huyu mkandarasi achunguzwe na ikithibitika amefanya makosa hatua za kisheria zichukuliwe,” alisema Masauni na kuongeza;

“Fedha zilizotumika ni nyingi halafu mkandarasi huyo eti anaondoka kwasababu ambayo inayojulikana akisingizia kuwa ukosefu wa fedha, Serikali haiwezi ikachezewa, tendo la kuchelewa kwa mradi huu ameitia hasara kubwa Serikali.”

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Mzee Nyamka alisema Mkandarasi huyo aliondoka mwaka jana kwa kuhamisha vifaa vyake na kuutelekeza mradi huo.
“Endapo mradi huu ungekamilika kwa wakati hakika mavuno ya mpunga yangeongezeka kwa kasi kubwa kutokana ukubwa wa mradi huu,” alisema Nyamka.

Akitoa taarifa yake kwa Naibu Waziri, Karani wa Mradi huo, Mkaguzi wa Jeshi hilo, katika Gereza la Kilimo Idete, Juma Mtega alisema kazi alizotakiwa Mkandarasi huyo kuzifanya ni kujenga jengo la ofisi litakalo tumika na mkandarasi na mhandisi mshauri, jengo la stoo ya kuhifadhia vifaa vya ujenzi na kujenga banio.

Pia alipaswa kujenga mfereji mkubwa wa kusafirisha maji kwenda mashambani umbali wa mita 2450, na kujenga mfereji mdogo wa kusafirishia maji mashambani umbali wa mita 3450. Hata hivyo, Mtega alisema mpaka mwaka jana alivyoondoka, kazi alizozifanya ni kujenga jengo la ofisi lenye vyumba vitatu ambalo bado halijakamilika, amejenga banio ambalo limekamilika kwa asilimia 95.

“Pia alifanikiwa kujenga mfereji mkubwa wa kusafirisha maji kwa umbali wa mita 2450 hadi 3250, hii inatokana na njia iliyotakiwa kupita mfereji ambapo awali ilibadilishwa. Pia amejenga mfereji mdogo wa kusafirishia maji umbali wa mita 150,” alisema Mtega.

Mwisho/-

No comments: