ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 12, 2017

Mchuano mkali wa urais Liberia

Monrovia, Liberia. Matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Jumanne nchini Liberia yamecheleweshwa kutangaza huku kuripotiwa kuwepo kwa mvutano uliohusisha vyama vikuu viwili vinavyochuana.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana hivi punde zimesema huenda matokeo hayo yakatangazwa leo Alhamisi huku kukiwa na mchuano mkali kati ya makamu wa rais Joseph Boakai na mwanasoka wa zamani George Weah.

Soma: Weah asema hatapokea matokeo ya kushindwa

Awali, chama tawala nchini humo kilitoa wito wa matokeo ya urais kusimamishwa kwa madai kuwa kumejitokeza dosari katika kura.

Chama hicho cha Liberty Party kimesema kinafikiria kuchukua hatua za kisheria dhidi ya tume ya uchaguzi ikiwa haitasikiliza madai yake.

Tume ya uchaguzi nchini humo inatarajiwa kutangaza mrithi wa Rais Ellen Jonhson Sirleaf.

Sirleaf ni rais wa kwanza mwanamke barani Afrika ambaye alishinda uchaguzi wa 2005 kufuatia kipindi cha mpito baada ya vita na baadaye alishinda tena 2011.

Makamu wa rais Boakai na mcheza soka wa zamani Weah ni wagombea wanaopewa nafasi kubwa kumrithi Sirleaf, ambaye kikatiba hawezi kuwania muhula mwingine.

Wapigakura milioni 2.18 walioandikishwa walipiga kura zao kumchagua rais kutoka idadi ya wagombea 20, ikiwa ni pamoja na mwanamke mmoja na kuwachagua wabunge 73 wa baraza la wawakilishi.

Iwapo kati ya wagombea hao hakuna atakayefikisha asilimia 50 wagombea wawili waliopata idadi kubwa watachuana tena kwenye duru ya pili itafanyika Novemba 7. Wachambuzi wa mambo wameashiria uwezekano wa uchaguzi huo kwenda duru ya pili.

MWANANCHI

No comments: