ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 27, 2017

PROF. ELISANTE AWAAGA WATUMISHI WA WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyevaa kaunda) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo leo mjini Dodoma ambapo awali ndiye alikuwa anaiongoza kabla ya mabadiliko ya safu ya Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Alhamisi tarehe 26 Oktoba, 2017. (Picha na Eleuteri Mangi-WHUSM, Dodoma)

Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante Ole Gabriel amewaaga watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo leo mjini Dodoma.

Prof. Elisante awali ndiye alikuwa anaiongoza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kabla ya mabadiliko ya safu ya Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Alhamisi Oktoba 26, 2017.

Prof. Elisante amewashukuru watumishi hao kwa ushirikiano waliompatia tangu alipoingia Wizarani hapo Aprili 01, 2012 akiwa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana, Naibu Katibu Mkuu na baadae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo. Idara ya Maendeleo ya Vijana kwa sasa ipo Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Tunapimwa kwa utendaji kazi, endelezeni utamaduni wa kuchapa kazi kwa kujituma, kushirikiana, kupendana na kuwajali watumishi wote hasa wa ngazi za chini” alisisitiza Prof. Elisante.


Aidha, amewataka watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa wabunifu ili utendaji kazi wao uwe wenye tija kwa wananchi wote watakao kuja kupata huduma wizarani hapo.

Kwa upande wa watumishi wa Wizara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Maedeleo ya Utamaduni Bi. Lilly Beleko amemhakikishia Prof. Elisante kuwa wataendelea kutumia fursa zilizopo kwa maedeleo ya Wizara na taifa kwa ujumla kwa kutumia ujuzi walionao kulingana na taaluma zao. 

Naye Mkurugenzi wa Sera na Mipango Petro Lyatuu amesema watamkumbuka Prof. Elisante kwa utendaji wake wa kazi kwa kujali muda, kila mara na alikuwa akiwasisitiza kutumia simu kimkakati kwa kupokea na kujibu simu ambapo kila mara alikuwa akisisitiza “Simu zenu mziweke kimkakati wakati wote”.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo sasa inaongozwa na viongozi wapya ambapo Katibu Mkuu wake ni Bi. Suzan Paul Mlawi na Naibu Katibu Mkuu akiwa Nicholaus B. William. 

No comments: