ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 27, 2017

Shirika la Hakizetu lazindua awamu ya pili ya mradi wa kutokomeza ukatili wa kijinsia Manispaa ya Ilemela

Binagi Media Group
Shirika la kutetea haki za wasichana na wanawake, Hakizetu lililopo Manispaa ya Ilemela Jijini Mwanza, limezindua mradi ujulikanao kama “Kila Mtu Aishi Vyema Kuanzia Sasa” awamu ya pili (Living Better Today Project  phase II), lengo ikiwa ni kutokomeza ukatili katika jamii.

Mradi huo umelenga kufanya kazi katika Kata mbili za Ibungiro na Nyamanoro katika Manispaa ya Ilemela ambapo vikundi mbalimbali vya kijamii vitaundwa hadi katika ngazi ya jamii na wanafunzi wa sekondari katika shule za Mwanza Baptis na Ibungiro na kujengewa uwezo kwa ajili ya kusaidia utoaji wa elimu ya kujikinga na ukatili wa kijinsia katika jamii.

Akizungumza jana kwenye uzinduzi wa mradi huo, Afisa Miradi wa shirika la Hakizetu, Gervas  Evodius alisema awamu ya kwanza ya mradi huo iliwafikia wananchi 2,400 katika wilaya ya Ilemela na Nyamagana hivyo awamu ya pili matarajio ni kuwafikia wananchi 300 ambao watakuwa mabalozi wa kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii.

Alisema mradi umelenga kufanya kazi zaidi katika ngazi za jamii/ familia ambapo kuna mzizi wa ukatili kwa wasichana na wanawake ikiwemo mimba na ndoa za utotoni na kwamba matarajio ni kutatua changamoto hiyo katika jamii.

Evodius alisema ni wakati mwafaka kwa wanajamii kuungana pamoja ili kutokomeza ndoa na mimba za utotoni pamoja kila aina ya ukatili wanaokumbana nao wasichana na wanawake kwani ni jukumu la kila mmoja kuwakinga.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Cunegunda Ngereja alisema shirika linatoa elimu pamoja na kuwawezesha kiuchumi wahanga wa ukatili wa kijinsia katika jamii ikiwemo kuwawezesha kiujasiriamli ili kuondokana na umaskini kwani umaskini na ukatili katika jamii huchangia mimba na ndoa za utotoni.

Alisema wanashirikiana na wadau mbalimbali kupitia vikao na kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha mtoto wa kike na wanamke wanakua salama katika jamii.

Mmoja wa washiriki wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo, Mwanasheria Akram Salim, alisema wanajamii wanapaswa kuelewa kwamba ukatili wa kijinsia katika jamii umepitwa na wakati hivyo ni vyema kuwa na mtazamo chanya wa kutambua kuwa kujihusisha na ukatili wa kijinsia ni kuvunja sheria za nchi.


Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkudi katika Kata ya Nyamanoro wilayani Ilemela, Salum Heri alisema baadhi ya watoto wa kike hukumbana na ukatili wakiwa nyumbani ikiwa ni pamoja mbimba za utotoni kutoka kwa watu wa karibu na hivyo sheria kushindwa kuchukua mkondo wake kutokana na kesi za aina hiyo kumalizwa kifamilia ambapo alitoa rai kwa shirika la Hakizetu kuendelea kuwasaidia kielimu na kiujasiriamli wasichana waliokumbana na ukatili wa aina hiyo ili kuwaondoa kwenye utegemezi katika jamii.

No comments: