ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 25, 2017

SHIRIKA LA PELUM TANZANIA LAWAPIGA MSASA WANAWAKE KUTAMBUA HAKI YA UMILIKI WA ARDHI

 Wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma wakifuatilia mafunzo kuhusu mpango wa matumizi bora ya ardhi yaliyokuwa yakitolewa na Maafisa kutoka Shirika la PELUM Tanzania hivi karibuni.
 Wanawake katika Halmashauri za Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma wakishiriki katika zoezi la kuanisha mipaka ya maeneo yao yatakayotumika katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo makazi, kilimo,biashara n.k lililofanyika hivi karibuni Wilayani humo.


Na Mwandishi Wetu,
WANAWAKE katika Halmashauri za Wilaya ya Kilolo na Mufindi Mkoani Iringa wamepongeza jitihada za Shirika la PELUM Tanzania za kuwapatia elimu ya mafunzo kuhusu Mipango ya Matumizi bora ya Ardhi Vijijini kwa kuwa hatua itawasadia kutambua haki walizonazo katika kumiliki, kutumia na kupata rasilimali ya ardhi.

Akizungumza hivi karibuni katika semina ya mafunzo ya mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa Wananchi Wilayani Kilolo,  Afisa Mipango Mji na Vijiji wa Wilaya ya Kilolo, Bernard Kajembe alisema kabla ya utekelezaji wa mradi wa CEGO suala la umiliki ardhi hususani kwa wanawake Wilayani humo ilikuwa ni jambo lisilopewa kipaumbile.
Kajembe alisema kuwa kwa kipindi kirefu mwanamke amekuwa akikosa haki yake ya kumiliki Ardhi kwa kigezo kuwa hana thamani kwenye familia aliyozaliwa na badala yake thamani yake ipo kwenye familia atakayoolewa na hivyo kupelekea mwanamke kuwa na jukumu la kutumia ardhi kwa ajili ya uzalishaji pekee.
“Tunalishukuru Shirika la PELUM Tanzania kwa kushirikiana na Halmashauri kutekeleza  mradi huu na kutoa elimu ya awali kuhusiana na masuala ya ardhi ambapo imetoa mwanya kwa wanawake kuanza kumiliki ardhi na hasa kwenye  vijiji vya mradi jambo ambalo kwa awali lilionekana ni kama uvunjaji wa mila na desturi” alisema Kajembe.
Kwa upande wake Bi. Maliamusi Mdalingwa mkazi wa kijiji cha Ugesa Wilayani  Kilolo alisema katika siku za nyuma ilikuwa jambo gumu kwa wanawake wengi ndani ya ndoa kumiliki hata kama ana haki ya kisheria kumiliki kwa makubaliano yao wawili. 
Anasema mara baada ya mafunzo kutoka Shirika la PELUM Tanzania kwa sasa hali imekuwa tofauti kwani anathamini hata haki za watoto wake wa kike kuwa nao wanapaswa kumilikishwa rasilimali ya ardhi.
Naye Bi. Agnes Mbamilo toka kijiji cha Isaula wilayani Mufindi alipongeza Shirika la PELUM Tanzania kwa kwa kuwapatia mafunzo hayo kwani yamesaidia kwa kiasi kikubwa kubadili fikra na mtazamo wa mume wake kwa sasa wana umiliki wa hati ya pamoja katika shamba na kiwanja cha nyumba.
Mbali na elimu ya Haki za ardhi kwa wanawake, mafunzo mengine yanayotolewa na Shirika la PELUM Tanzania ni pamoja na elimu juu ya Mpango wa matumizi ya Ardhi kijijini, Haki ya kupata, kutumia na kumiliki Ardhi Tanzania, Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Tanzania pamoja na Utawala wa Kidemokrasia katika Jamii. 
Mafunzo hayo yanatolewa kupitia mradi wa ushiriki wa wananchi kwenye Sekta ya kilimo (CEGO) na kufadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) yalitolewa katika vijiji 10 vya Wilaya hizo.

No comments: