ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 30, 2017

UNDANI KUHUSU SHEREHE ZA HALLOWEEN KILA IFIKAPO OKTOBA 31

Na Jumia Travel Tanzania

Inawezekana utakuwa umesikia watu au kusoma kwenye mitandao ya kijamii kuhusu sherehe za Halloween lakini ukawa hauelewi. Mbali na hapo inawezekana pia umekutana na matangazo kadhaa yakikutana kushiriki kwenye sherehe za sikukuu hiyo sehemu kadhaa za starehe hususani vilabu vya usiku hapa nchini.
Kutokana na utandawazi uliosababisha dunia kuwa kijiji tumejikuta kwa namna moja ama nyingine tukishiriki matukio mbalimbali kwa wakati mmoja. Baadhi ya matukio hayo huwa hatuelewi maana yake kwa undani zaidi. Kwa mfano, Halloween kwa namna inavyosherehekewa ni kama ina uhusiano na sherehe za kishetani.

Ikiwa sehemu mbalimbali duniani zimeshaanza maandalizi ya sherehe za Halloween ambazo hufanyika kila ifikapo Oktoba 31 ya kila mwaka, Jumia Travel ingependa kukufahamisha juu ya maana halisi ya sherehe hii.  
Japokuwa umaarufu wa sherehe ya Halloween umetokana na nchi ya Marekani lakini ukweli ni kwamba wanahistoria wanaamini sherehe hii ilianzia nchini Ireland na kusambaa nchi za jirani za Scotland, Uingereza, Ufaransa na baadaye sehemu zingine duniani.

Na kudhihirisha kwamba Marekani inasherehekea sherehe hii kikamilifu, inaaminika kwamba ni sherehe ya pili kwa ukubwa wa kibiashara ndani ya mwaka. Katika kipindi hiki takwimu zinaonyesha kwamba wamarekani hutumia zaidi ya dola bilioni 5 kuadhimisha sherehe hii. Na kwa kuongezea robo ya mauzo yote ya peremende au pipi ya mwaka hufanyika ndani ya kipindi hiki nchini humo.
Halloween ina maana gani na kwanini husherehekewa kila ifikapo Oktoba 31 ya mwaka?

Maana halisi ya neno Halloween ni siku ya mkesha wa siku ya watakatifu wote ambayo huadhimishwa kila ifikapo Novemba mosi. Halloween pia ni ufupisho wa neno ‘Allhalloween, All Hallows’ Evening na All Saint’s Eve’ ambapo husherehekewa kila ifikapo Oktoba 31 ya kila mwaka.

Asili ya Halloween ilitokana na sherehe ya ‘Samhain’ iliyokuwa ikiadhimishwa na watu wa kale wa Ireland au ‘Waseltiki’ kama wanavyojulikana.

Samhain ni sherehe ya wapagani wa kiseltiki ikimaanisha ‘Mwisho wa Majira ya Joto’ ambayo huadhimishwa mwisho wa msimu wa mavuno.

Hiki kilikuwa ni kipindi ambacho walikuwa wakiwasha moto kuuzunguka na kisha kuvalia mavazi yanafanana na ya mashetani ili kuepekana na mizimu inayosemekana huwa inarandaranda usiku huo.

Katika karne ya nane, Papa Gregory III alisema kwamba Novemba mosi itakuwa ni siku ya kuwakumbuka watakatifu na wafia dini wote. Na hapo ndipo ‘Siku ya Watakatifu Wote’ ilipoanzia na jioni yake ilikuwa ikijulikana kama ‘All Hallows’ Eve’ na baadaye kuwa Halloween.
Halloween imepata umaarufu mkubwa kadiri muda unavyokwenda na kuwa kipindi cha kufanya biashara kwa wingi ambapo watoto na watu wazima husherehekea kwa kuvalia mavazi ya kuogofya kama mizimu au mashetani na kwenda kuhudhuria sherehe zinazoandaliwa.

Kwanini watu huvalia mavazi ya kuogofya usiku wa Halloween?

Utamaduni ambao umekuwepo kwa miaka mingi katika kusherehekea Halloween ni pamoja na kuvalia mavazi ya kutisha kama mizimu au mashetani.
Washerehekeaji hufanya hivyo kutokana na asili ya sherehe hii ambapo inaamini kwamba katika mkesha wa siku ya Oktoba 31 kuamkia Novemba mosi mashetani, wachawi na mizimu huwa inarandaranda mitaani kusherehekea kuanza kwa msimu wao - kipindi cha majira ya baridi. Inasemekana kwamba huranda mitaani na kuwachezea watu, kuwatisha, kuwadhuru na kuwafanyia hila mbalimbali kadiri wanavyopenda.

Njia pekee kwa watu waliokuwa wanaogopa kutishwa na mizimu hiyo ni kuwapatia vitu ambavyo walikuwa wanavipendelea, mara nyingi huwa ni vyakula vitamu na zawadi nzuri kama vile peremende kwa kuviacha milangoni.

Au, njia nyingine iliyokuwa ikitumika, kwa watu ambao walikuwa wanaogopa, ni kwa kuvalia mavazi kama yao na kisha kurandaranda mitaani, lengo ni kwa mizimu hiyo kutowatambua na kuwafananisha binadamu hao na wenzao.

Je unajiuliza kama usherehekee sikukuu ya Halloween? Kumekuwa na dhana tofauti juu ya sherehe hii ambayo kwa namna moja ama nyingine zimekuwa zikihusishwa na ushetani na ushirikina. Hii inategemea namna wewe mwenyewe utakavyosherehekea na kwa malengo gani na kama itaathiri vipi imani yako. Kwa makala haya, Jumia Travel inaamini kwamba utakuwa umefahamu machache kuhusiana na sherehe hii ambayo inazidi kushika kasi kadiri miaka inavyokwenda.

No comments: