Watu wawili wamefariki dunia na mwingine mmoja kujijeruhi baada ya kutokea ugomvi unaohusishwa na wivu wa mapenzi mjni Bunda.
Tukio hilo lilitokea jana saa tano asubuhi katika Mtaa wa Bunda Stoo baada ya mtu mmoja kuwavamia watu wawili kisha kuwachoma visu kabla ya kujichoma mwenyewe.
Akizungumza mjini hapa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Jaffari Mohamed alisema jana kuwa waliouawa ni Daudi Phares (29) mkazi wa Bunda na msichana aliyetambulika kwa jina moja la Monica (22) mkazi wa Magu mkoani Mwanza.
Kamanda huyo alimtaja aliyejijeruhi baada ya kujichoma kisu maeneo mbalimbali mwilini mwake kuwa ni Selemani Jeremia (33) ambaye ni mkazi wa Magu.
Alisema kuwa siku ya tukio Selemani alisafiri kutoka Magu mkoani Mwanza hadi Bunda ambapo alifika nyumbani kwa Daudi na kumkuta akiwa na Monica.
Baada ya kufika nyumbani hapo Selemani alianza kumchoma visu Dauidi katika sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwamo kifuani upande wa kushoto na kusababisha kifo chake papo hapo.
Alisema kuwa baadaye Selemani alianza kumshambulia Monica ambapo alimkata kwa kisu shingo hadi ikaning’inia na baadaye kumchoma sehemu mbalimbali hali iliyomsababishia mauti palepale.
Kwa mujibu wa Kamanda Mohamed mtuhumiwa alitaka naye kujiua kabla ya kuokolewa na polisi na wananchi waliofika eneo la tukio waliomkuta amejikata na kisu shingoni na kujichoma tumboni hali iliyosababisha utumbo wake kutoka nje.
“Selemani pamoja na kujichoma huko alikutwa akiwa bado anapumua na kukimbizwa katika Hospitali Teule ya Bunda ambapo alipatiwa matibabu na sasa hivi bado yuko hospitalini ingawa hali yake si nzuri,” alifafanua.
Kamanda huyo alisema kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa tukio hilo linahusishwa na wivu wa mapenzi kwa maelezo kwanza miezi michache iliyopita Monica na Selemani walikuwa wachumba ambapo Selemani alitoa kishika uchumba nyumbani kwao Monica na kwamba walikuwa na mpango wa kuoana punde.
Lakini kabla hawajafikia malengo yao, Monica alibadili uamuzi na akaenda Bunda ambapo alianza kuishi pamoja na Daudi hali iliyosababisha ndugu wa Monica na Selemani kuingilia kati na hatimaye Monica kurudishwa wilayani Magu.
Hata hivyo, licha ya kurudishwa Magu lakini uchumba wao ulivunjika rasmi na familia yake kurudisha kishika uchumba kwa Selemani.
Taarifa zaidi zilisema baada ya uchumba huo kuvunjika, Monica aliamua kurudi tena wilayani Bunda na kuendelea kuishi na Daudi na ndipo Selemani aliamua kumfuata na kutekeleza tukio hilo lililowaondolea uhai wapenzi hao.
No comments:
Post a Comment