ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, October 8, 2017

AUAWA KWA KUPIGWA MSHALE WENYE SUMU TARIME


Jeshi la polisi mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya

linawashikilia watu 18 kwa tuhuma za mauaji ya mtu  mmoja aliyefahamika kwa jina la Magige Mesenda 32 mkazi wa kijiji cha  Nyarwana Kata ya Kibasuka Wilayani Tarime Mkoani Mara.

Akizungumza na waandishi wa habari leo,Kamanda wa polisi Mkoa wa Polisi Tarime Rorya SACP Henry Mwaibambe amesema Magige aliuawa kwa kushambuliwa na mshale wenye sumu  katika paja lake la mguu wa kulia na wananchi ambao waliotambuliwa kwa sura wakazi wa kijiji cha Matongo ambao walitoroka baada ya kufanya  tukio hilo.

Aliongeza kuwa kabla ya tukio hilo watuhumiwa walimkamata mtoto wa  marehemu aliyefahamika kwa jina la Mwita Magige (11) mwanafunzi wa  darsa la tatu akiwa anachunga mifugo ya baba yake na kumnyanganya simu 
na radio ndogo kisha kupora mifugo.

Kufuatia tukio hilo mtoto huyo alitoa taarifa kwa baba na marehemu alifika eneo la tukio akiwa na baadhi ya  wanakijiji kujua kulikoni na ndipo alishambuliwa kwa mshale na mauti  kumkuta.

"Kiini cha vurugu ni mgogoro ambao ulishatatuliwa siku nyingi juu ya nani  anamiliki mto Tigite kati ya wanahi wa kijiji cha Matongo na Nyarwana  ambapo iliamuliwa kila upande una haki ya kutumia mto huo" ,alisema 
Kamanda.

Aidha kamanda amezitaja silaha za jadi zilizokamatwa  kufuatia tukio hilo kuwa ni mishale 46 pinde 10 na mkuki mmoja na kusema kuwa jeshi la polisi litahakikisha linawakamata  watu wote waliohusika katika tukio hilo.
Kamanda wa polisi Tarime Rorya SACP:Henry Mwaibambe akionyesha baadhi ya silaha za jadi ikiwemo Mishale, Upinde na Mkuki zilizokuwa zikitumika katika mapigano hayo.
PICHA ZOTE NA CLEO24NEWS

No comments: