Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri akihamasisha ulimaji wa zao la Pamba kwa wakulima wa Wilaya ya Urambo Mkoani humo wakati wa ziara yake ya kikazi kuhamishisha shughuli za maendeleo.
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Urambo Mkoani
Tabora wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa mkoa huo Aggrey Mwanri alipofanya ziara
katika wilaya hiyo kuhamasisha shughuli za maendeleo ikiwe kilimo cha zao la
Pamba. (Picha na: RS- Tabora)
Na: Tiganya Vincent.
BODI ya Pamba Tanzania imetakiwa kuongeza mbegu
za pamba kufuatia wakazi wengi wa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Tabora
kujitokeza kwa wingi kutaka kulima zao hilo katika msimu wa kilimo ulianza hivi
karibuni.
Kauli hiyo ilitolewa jana Novemba 28, 2017 na Mkuu wa
Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa mkutano wake na wanavijiji wa Wilaya ya
Urambo waliojitokeza na kumweleza kero mbalimbali ikiwemo uhaba wa kuwa mbegu za
pamba kufuatia wengi wao kuonesha nia ya kulima zao hilo.
Alisema kuwa baada wakulima wengi kupatiwa elimu ya
uhamasishaji juu ya kilimo cha kisasa cha zao hilo ikiwemo uzingatiaji wa sheria
na kanuni za ulimaji wa pamba kumekuwepo na mwitikio mkubwa wa wanakijiji
kutaka kulima zao hilo.
Mwanri alisema kuwa si vema kuwakatisha tamaa wakulima
hao kwa sababu ya ukosefu wa mbegu na dawa za kuua wadudu, hivyo ni vema Bodi ikalishughulikia suala hilo kwa
haraka zaidi.
“Bodi nawaombeni sana msije mkanifanya nionekane
mwongo kwa kuwaambia wakulima kuwa mbegu zitapatikana na kisha zisifike
…hawataniamini tena” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Alisema kuwa Mkoa wa Tabora ndio uliochaguliwa kuwa
mzalishaji wa mbegu za pamba na kitalu cha taifa kwa ajili ya maeneo
mengine nchini, hivyo mbegu pekee inayohitajika kupandwa ni UKM08 katika maeneo
yote.
Mwanri alitoa wito kwa Bodi hiyo kuhakikisha kuwa
upungufu wa mbegu hizo unaondolewa na zinawafikia wakulima mapema kwa sababu
mvua zimeshaanza kunyesha na kuna baadhi ya maeneo mkoani humo zinakuwa ngumu
kupitika katika kipindi hicho.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Urambo Angelina Kwingwa
alisema kuwa katika msimu ujao wa kilimo makisio yao ilikuwa kupokea tani 31,020
lakini hadi sasa wamepokea tani 19,398 na kusambazwa katika vijiji 56
kati ya 57 vilivyokisiwa kulima zao hilo.
Alisema kulingana na hamasa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa
katika maeneo mbalimbali wakulima wengi wamehamasika ambapo wameongezeka kutoka
4,268 hadi kufikia 4,689.
Kwingwa alisema kuwa hali hiyo inawafanya wanahitaji
nyongeza ya tani 36 za mbegu ili waweze kukamilisha kwa wakulima wote.
Naye Meneja wa Bodi ya Pamba Tanzania, Kanda ya
Magharibi Jones Bwahama alisema kuwa hakuna mkulima ambaye hatashindwa kulima
zao hilo kwa sababu ya kukosa mbegu za pamba.
Alisema kuwa nyongeza ya mbegu za pamba zimeshaanza
kupelekwa katika maeneo ambayo makisio yameongezeka na zitawafikia wakulima
wakati wowote kuanzia sasa.
Bwahama aliongeza kuwa wakati wakiendelea kusambaza
mbegu katika maeneo ambayo yanakabiliwa na upungufu, Kampuni ya Usambazaji Mbegu ya Quoton Tanzania
Limited iliyopewa jukumu la kuandaa mbegu za pamba mkoani humo inaendelea
na zoezi la kuandaa mbegu zaidi ili kukabiliana na upungufu utakaojitokeza.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Urambo Adam Malunkwi alitoa rai kwa wakulima kuzingatia maelekezo ya Mkuu wa
Mkoa ili waweze kulima na kuzalisha mazao bora.
No comments:
Post a Comment