Rais Adama Barrow, mwishoni mwa wiki iliyopita, aliamua kuhamia rasmi ikulu ikiwa ni miezi 10 tangu alipoapishwa kuongoza nchi hiyo ndogo iliyoko magharibi mwa Afrika.
Barrow kwa kipindi chote hicho alikuwa anaishi hotelini kabla ya kuhamia katika ikulu iliyoko mji wa Fajara. Picha zilizosambazwa na wanahabari kupitia mtandao zinaonyesha Barrow akiwasili katika eneo hilo ambako liliandaliwa gwaride la heshima kwa ajili yake.
Tangu mtangulizi wake Yahya Jammeh alipoondoka Januari, majengo hayo yalidaiwa kuwa si salama kwa Barrow ikidaiwa zilifichwa bunduki na silaha za kemikali. Jammeh kwa sasa anaishi uhamishoni Equatorial Guinea alikokimbilia baada ya kulazimishwa kutoka madarakani.
Majeshi ya Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) yaliyaweka majengo hayo chini ya ulinzi na kufanya upekuzi ili kuhakikisha usalama wa kutosha kabla ya mamlaka huzika kuyafanyia matengenezo kisha kuruhusu Rais Barrow ayatumie.
Jammeh aliangushwa katika uchaguzi mkuu wa Desemba 2016 na Barrow aliyegombea kwa muungano wa upinzani. Kwanza Jammeh aliridhia matokeo ya kushindwa kwake lakini mara alibadili kauli akatangaza kuyafuta akitaja dosari kadhaa. Ecowas waliingilia kati huku Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari akiongoza usuluhishi na ndipo alikimbilia huko aliko sasa.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment