Katibu mkuu wa Wizara ya Viwanda ya Biashara na Uwekezaji, Prof Elisante Ole Gabriel akiwa katika ziara ya kikazi nchini China (Beijing) ametembelea kiwanda cha Huanri Medical Group kinachojishughilisha na utengenezaji wa vifaa tiba, Mitungi ya Gesi na Matairi.
Akiwa kiwandani hapo alishuhudia baadhi ya Vifaa vya tiba vinavyongenezwa kiwandani hapo Fingertip/Handheld Oximeter ambacho hutumika kupima kiwango cha hewa ya Oxygen katika damu (vinawafaa zaidi wakina mama waja wazito na wazee), Anesthesia Machine inayotumika katika upasuaji mkubwa pale ambapo mtu amewekewa dawa ya usingizi, Ventilator inayotumika ICU kwa ajili ya kusaidia upumuaji kwa mgonjwa aliyezidiwa pamoja na Kifaa kinachofahamika kama Health Machine (Mfano wa Briefcase) kilichotengenezwa mahususi kwa ajili ya soko la bara la Afrika na kinaweza kutibu takribani magonjwa 16 na kinabeba vifaa vingi ndani yake.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda,Biashara na Uwezeshaji Prof. Elisante Ole Gabriel akishiriki katika kuunganisha Mashine inayofahamika kama "Anesthesia Machine" inayotumika katika usaidizi wa shughuli za Upasuaji Mkubwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwezeshaji Prof. Elisante Ole Gabriel (Katikati) pamoja na ujumbe alioambatana nao, alipotembelea kiwanda cha Huanri Medical Group jijini Beijing nchini China.
Akieleza lengo la kutembelea kiwanda hicho Prof. Elisante alisema ni kuzibaini fursa za uwekezaji zilizopo na jukumu la wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ni kuhakikisha kwamba wanajenga mazingira ya ya wawekezaji kuwekeza vizuri bila kupoteza muelekeo na lengo kubwa la kuinua Uchumi wetu. “tungependa tuwe na mikataba ambayo kwa vyovyote vile hata kizazi kijacho kikija kuangalia hayo makubaliano kifurahi na kuthamini kwamba waliongia katika makubaliano waliona mbele na walijali maslahi mapana ya taifa.
Tunachoamini ni kwamba wenzetu hawa wachina katika tasnia mbalimbali watakuja Tanzania watawekeza, jukumu letu kubwa sisi na tunachokifanya ni kuendelea kuwavutia kuwaweka katika mlengo ambao watafanya kazi zao vizuri katika mazingira wezeshi na rafiki ili mwisho wa siku ajira ziongezeke katika nchi yetu ya Tanzania lakini pia tuweze kuuza vifaa vingi sana kutoka Tanzania kwenda kwenye masoko ya nje kwa ajili ya kupata fedha za kigeni lakini lingine ambalo ni siri kubwa ya mafanikio ni kupata pia utaalam ili vijana wa kitanzania waweze kupata taaluma hii ambayo ni ya kiwango cha juu” Alisema Prof. Elisante.
akifanya mahojiano na vyombo vya habari baada ya kuhitimisha ziara yake kiwandani hapo
Akitazama moja ya hatua za kutengenezaji wa Vifaa vya Tiba kiwandani hapo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante Ole Gabriel akisalimiana na Rais wa Kampuni ya Huanri Medical Group Bw. Wang qianjun Mara baada ya kuwasili kiwandani hapo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof.Elisante Ole Gabriel akizungumza jambo na Viongozi kutoka China - Asia Economic Development Association Overseas Cooperation Committee, alioambatana nao Kiwandani hapo.
Akionyesha furaha yake Katibu Mkuu alisema tayari Huanri Medical Group wamekubali walau kwenye masuala ya taaluma ya vifaa tiba wataweza kuwaalika vijana wetu wa kitanzania waje wakae China kwa takribani miezi mitatu ili wapate utaalam wa kuunganisha vifaa hivi vya tiba lakini lengo la serikali yetu ni kuona kiwanda hiki kikijengwe Tanzania na hatua hii itapanua wigo wa ajira na pato la taifa litazidi kuongezeka.
“ Huanri Medical Group ni miongoni mwa kundi kubwa la wawekezaji wanaotarajia kuja Tanzania Mwezi Machi 2018 kwa ajili ya mikutano mbalimbali ya uwekezaji na sisi tunawahakikishia kwamba serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dr. John Pombe Magufuli inawakaribisha sana, na imani yetu ni kwamba Changamoto ya ajira itaweza kupungua pale tutakapoendelea kuleta wawekezaji nchini.” Alisema Prof Elisante.
Akihitimisha ziara hiyo katika kiwanda hicho Prof. Elisante amewataka watanzania kuendelea kupenda vitu vinavyozalishwa katika Taifa letu na kununua vitu vyetu vya ndani. Amesema jambo la muhimu na kubwa ni upatikanaji wa uhamisho wa technolojia kutoka China na kwamba tayari Tanzania imeahidi kufanya kazi na wawekezaji hao kwa ushirikiano kwa lengo la kuhakikisha ndoto na falsafa hii ya serikali ya awamu ya tano inakamilika na kufikiwa kwa kwa kasi nzuri.”
Kwa upande wake Rais wa kampuni hiyo ya Huanri Medical Group Bw. Wang qianjun amefurahishwa na juhudi ambazo zinafanywa na Serikali ya Tanzania kwenye sekta ya viwanda na ameahidi ushirikiano mkubwa na kuonyesha utayari wake wa kuwekeza Tanzania .
Katika ziara hiyo Katiba Mkuu wa Wizara ya Viwanda,Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante Ole Gabriel aliambatana na Afisa Mwandamizi wa Ubalozi wa Tanzania nchini China Said Massoro, Viongozi kutoka China - Asia Economic Development Association Overseas Cooperation Committee (Naibu Katibu Mkuu Bi. Rui LU na Makamu wa Rais Bi. Tian Wenhui) Bw.Remidius Emmanuel Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wanafunzi Watanzania nchini China pamoja Bi. Muka Kamuzora Mtanzania anayesoma Masuala ya Uchumi hapa China.
No comments:
Post a Comment