ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 29, 2017

SHILINGI BILIONI 375.4 ZATOLEWA KUONDOA TATIZO LA MAJI MKOA WA SIMIYU

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe aliongoza kikao cha wadau kujadili mradi wa maji katika halmashauri za  Mkoa wa Simiyu. Tayari tahmini ya mazingira imekamilika na kazi ya upembuzi yakinifu ipo katika hatua za mwisho na zabuni imepangwa kutangazwa mwezi Januari 2018 baada ya kukamilika kwa zabuni, Ujenzi wa Mradi unakadiriwa kuchukua miezi 24.

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira iliwasilisha ombi la fedha kwa Mfuko wa Global Climate Fund (GCF) ili kutekeleza Mradi wa maji katika halmashauri zilizopo Mkoa wa  Simiyu unaojulikana kama Simiyu Climate Resilience Water Supply Project. Kuibuliwa kwa Mradi huu kulitokana na uhitaji mkubwa wa maji katika Mkoa wa Simiyu kulikosababishwa na ukame wa muda mrefu.

Mradi huu, umepangwa kutekelezwa kwa awamu mbili katika Wilaya tano za Mkoa wa Simiyu. Wilaya hizo ni Busega, Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu. Katika Awamu ya kwanza, Mradi utatekelezwa katika Wilaya za Busega, Itilima na Bariadi. Kiasi cha Euro milioni 140.7 sawa na takriban shilingi bilioni 375.4 zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha utekelezaji wa mradi huo.


Fedha za kutekeleza Awamu ya Kwanza ya Mradi zitachangiwa na Serikali ya Tanzania na Washirika wa Maendeleo ambao ni GCF na Serikali ya Ujerumani. GCF watachangia Euro Milioni 102, Serikali ya Ujerumani watachangia Euro Millioni 25.6 na Serikali itachangia Euro Millioni 13.1 na wananchi nao kupitia nguvu zao watachangia Euro Millioni 1.5. Matumizi ya Fedha za GCF na Serikali ya Ujerumani yatasimamiwa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW).

Lengo kuu la Mradi ni kuboresha afya na kuongeza uzalishaji mali ili kuinua hali ya maisha ya wananchi walioathirika na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo husika ya Mradi.

Kukamilika kwa mradi huu kutawezesha upatikanaji wa huduma ya maji ya uhakika kwa kujenga mfumo wa uzalishaji na usafirishaji maji na kuboresha mfumo wa usambazaji wa maji katika miji na vijiji husika.

Mradi pia utahusisha kujenga kwa mabwawa ya kilimo cha umwagiliaji endelevu (Smart Agriculture) ambayo pia yatatumika kunyweshea mifugo pamoja na kuimarisha huduma za usafi wa mazingira kwa kujenga mabwawa ya kukusanyia na kuchuja majitaka na vyoo vya mfano mashule na vituo vya afya.

No comments: