Meza Kuu wakiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kushoto) wakiimba Wimbo wa Taifa wakati wa Mahafali ya 43 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha- IFM, yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Jijini Dar es Salaam ambapo wanafunzi 2692 wamehitimu kozi mbalimbali katika Nyanja za Fedha, Uhasibu, Bima, TEHAMA na Hifadhi ya Jamii. Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho Prof. Lettice Rutashobya na wa Pili kulia ni Mkuu wa Chuo hicho Prof. Tadeo Satta.
Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha-IFM, Prof. Tadeo Satta, akihutubia wakati wa Mahafali ya 43 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha- IFM, yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Jijini Dar es Salaam, ambapo wanafunzi 2692 wamehitimu kozi mbalimbali katika nyanja za fedha, uhasibu, bima, TEHAMA na hifadhi ya jamii.
Mwenyekii wa Baraza la Chuo cha Usimamizi wa Fedha-IFM, Prof. Lettice Rutashobya, akihutubia wakati wa Mahafali ya 43 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha- IFM yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Jijini Dar es Salaam, ambapo wanafunzi 2692 wamehitimu kozi mbalimbali katika nyanja za fedha, uhasibu, bima, TEHAMA na hifadhi ya jamii.
Baadhi ya wahitimu wa Mahafali ya 43 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha- IFM, yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Jijini Dar es Salaam, wakifuatilia kwa makini matukio yaliyokuwa yakiendelea wakati wa mahafali hayo ambayo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb).
Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 43 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha- IFM yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Jijini Dar es Salaam, Dkt. Philip Isdor Mpango Mb), akihutubia Jumuiya ya wanachuo hicho ambapo aliwatunuku vyeti wanafunzi 2692 waliohitimu kozi mbalimbali katika nyanja za fedha, uhasibu, bima, TEHAMA na hifadhi ya jamii.
Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha-IFM, waliofanya vizuri zaidi katika masomo yao wakipokea zawadi ya hundi kifani yenye thamani ya shilingi 1,200,000 ambayo ni sehemu ya zawadi lukuki walizopewa wakati wa Mahafali ya 43 ya Chuo hicho, yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Jijini Dar es Salaam.
Mhitimu Bi. Elizabeth Mnzava akipokea zawadi ya cheti kutoka kwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 43 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha IFM, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) baada ya kufanya vizuri katika masomo yake.
Sehemu ya wahitimu wa Mahafali ya 43 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha-IFM, wakinyanyua juu kofia zao kwa furaha kuashiria kumaliza sehemu ya safari yao ya kimasomo, baada ya kutunukiwa vyeti na shahada nyingine mbalimbali, katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa wahitimu ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja akionesha furaha isiyo kifani baada ya kutunukiwa Shahada yake baada ya kuhitimu masomo katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha-IFM, Jijini Dar es Salaam, ambapo Mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb).
Sehemu ya wahitimu wa Mahafali ya 43 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha-IFM, wakinyanyua kofia zao juu kwa furaha baada ya kutunukiwa shahada zao wakati wa mahafali hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amewaonya wahitimu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha IFM kuacha tamaa ya kutaka kupata mali za haraka haraka na kutojihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi wawapo kazini ili waweze kuisadia nchi kufikia maendeleo ya haraka.
Dokta Mpango aliyasema hayo wakati akiwatunuku vyeti vya kozi mbalimbali wahitimu 2692 wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha IFM, wakati wa mahafali ya 43 ya Chuo hicho yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa moja ya changamoto zinazoikabili jamii hivi sasa ni mmomonyoko wa maadili katika utumishi wa Umma hali iliyosababishwa na suala la rushwa na ufisadi kuota mizizi na kuwa tatizo kubwa katika jamii.
"Katika miaka ya karibuni kumekuwa na matatizo mengi ya matumizi mabaya ya fedha za umma ikiwemo watumishi hewa, wanafunzi hewa na pembejeo hewa, nawataka wahitimu mkafanyekazi zenu kwa kuzingatia maadili na kuepuka tabia ya kutaka utajiri wa harakaharaka” Alisisitiza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango alitumia fursa hiyo pia kuelezea mafanikio makubwa yaliofikiwa nchini katika sekta ya fedha katika kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma, mikopo ya mitaji ya kuwekeza katika Sekta mbalimbali na kuhakikisha kuwa sekta hiyo inabaki imara.
Alisema kuwa kutokana na hatua hizo, idadi ya taasisi za fedha imeongezeka kutoka 31 zilizokuwepo mwaka 1999 hadi kufikia 67 Novemba mwaka 2017 huku taasisi hizo zikiwafikia watu wengi zaidi hadi pembezoni mwa miji hata vijijini.
"Sekta ya Bima nayo imepiga hatua ambapo kampuni zilizosajiliwa zimefika 31, wakala wa bima 124 kutoka wakala 1 iliyokuwepo miaka ya 70 huku ukwasi katika kampuni hizo ukiongezeka kutoka asilimia 47.1 mwezo Juni 2016 hadi kufikia asilimia 49.8 mwezi Juni, 2017.
Alisema kuwa licha ya mafanikio hayo, taasisi za fedha zimekuwa zikiathiriwa na uwepo wa mikopo chechefu iliyoongezeka hadi kufikia asilimia 10.74 mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 9.07 mwaka 2016 na kutoa wito kwa wahitimu hao kubuni mikakati ya kukabiliana na changamoto kama hizo na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwa kuzingatia mahitaji ya Taifa ili kuondokana na umasikini.
Aidha, Dokta Mpango alisema kuwa Serikali itaendelea kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu wenye uhitaji ambapo katika Bajeti ya Mwaka huu, imepanga kutumia zaidi ya shilingi bilioni 427.54 kwa kazi hiyo kwa kuwalipia ada na gharama nyingine za masomo wanafunzi 122,623.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Usimamizi wa Fedha IFM Prof. Lettice Rutashobya ameiomba Serikali kukisaidia Chuo hicho kwa kukipatia fedha ili kiweze kujiimarisha na kuendelea kutoa taaluma bora ya masuala ya fedha, uhasibu, bima, TEHAMA na Hifadhi ya jamii huku Mkuu wa Chuo hicho Prof. Tadeo Satta akisema kuwa chuo hicho kimejipanga kujenga kampasi mkoani Pwani na mkoani Dodoma ikiwa ni mikakati ya kuongeza uwezo wa kudahili wanafunzi wengi zaidi.
Aidha viongozi hao wa Chuo cha IFM waliiomba Serikali kutenga shilingi bilioni 2 kila mwaka katika Bajeti ya Serikali ili waweze kuzitumia kujenga kampasi hizo mbili, moja katika eneo la Msata mkoani Pwani na nyingine inayotarajiwa kujengwa mkoani Dodoma.
“Katika hatua za awali wakati tunataka kutumia eneo la ekari 50 tulilolipata mkoani Dodoma, Chuo kimepanga kuanza kutoa mafunzo ya shahada ya uzamili katika fani ya fedha na uwekezaji kwa kutumia miundobinu ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini mkoani Dodoma.
Chuo cha Usimamizi wa Fedha IFM kilianzishwa mwaka 1972 kikianza na kozi mbili na kutoa wanafunzi 75 lakini hivi sasa chuo hicho kinatoa kozi 23 ambapo mwaka huu wahitimu 2692 wamemaliza masomo yao.
No comments:
Post a Comment