Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, leo Jumatatu, Novemba 27, 2017 amefunguka kuwa, chama chao wameshapata matokeo ya kata zote walizoshiriki uchaguzi mdogo wa madiwani ulifanyika jana Jumapili huku akisema hawajashinda hata kata moja.
Adiha kiongozi huyo amelaani vitendo vya vurugunna fujo vilivyofanywa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura na kusababisha taharuki miongopnmi mwa wapiga kura.
“Uchaguzi wa Madiwani Umekwisha, ACT Wazalendo, tunalaani vurugu na Kuwashukuru Watanzania. Jana tumemaliza Uchaguzi mdogo wa madiwani nchi nzima. Katika kata zote 43 nchini zilizogombewa, Sisi ACT Wazalendo tuliweka wagombea kwenye kata 17 tu.
“Tumepata matokeo ya kata zote na hakuna kata tuliyoshinda. Wapiga kura wameamua na sisi tumekubali. Tunafanya tathmini ya matokeo nchi nzima na tutazungumza na Wananchi. Tunawashukuru sana kwa kura tulizopata. Tutazienzi kwani ndio haki yetu.
“Tunajiandaa na chaguzi ndogo zinazokuja ikiwemo za Ubunge kwenye majimbo yaliyowazi. Tutatumia mafunzo tuliyoyapata kwenye chaguzi ndogo hizi kujipanga na chaguzi zinazokuja.
“Kwetu sisi Chama cha Wazalendo, Uchaguzi ulikuwa fursa ya kuzungumza na Wananchi na kufikisha ujumbe wetu kwani kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara kunatunyima fursa hiyo. Hatutachoka kuendelea kusambaza sera zetu kwani tunaamini ni bora zaidi na zinazoweza kuleta unafuu kwa wananchi
“Mwezi mmoja huu wa kampeni, tumepita sehemu mbalimbali za nchi na kuzungumza na Wananchi, kusikiliza matumaini na changamoto zao na kuwaeleza hali ya nchi kisiasa na kiuchumi. Tumeweza kufikisha ujumbe wetu wa kampeni za mwaka huu zilizojikita kwenye masuala ya Haki na Uchumi
“Tumewaeleza namna haki za raia zinavyominywa na namna Uendeshaji mbovu wa uchumi unavyowaweka kwenye dimbwi la umasikini. Tumewaeleza namna uhuru wa mawazo unaminywa, vyama kuzuiwa kufanya mikutano kueneza sera zetu.
“Bunge kuzuiwa kuonyeshwa moja kwa moja ili Wananchi kufuatilia namna wanavyowakilishwa na magazeti kufungiwa ili kudhibiti uhuru wa Habari.
“Tumewaeleza kuhusu vitendo vya kinyama vya kushambulia wawakilishi wa Wananchi kwa lengo la kuua na kufungulia kesi wanasiasa wanaoikosoa Serikali na kutoa mawazo mbadala.
“Yote haya yanafanywa kwa lengo la mtu mmoja kudhibiti mamlaka ya nchi na kufanya ukiritimba wa Uendeshaji wa nchi yetu jambo ambalo ni hatari kwa Demokrasia yetu.” amesema Zitto Kabwe.
No comments:
Post a Comment