Advertisements

Friday, December 15, 2017

Aliyefungwa akiwa miaka 12 afunguka

PEKOS Mtalikidonga (55) mfungwa aliyekuwa na umri mdogo kuhukumiwa kunyongwa akiwa na wenzake wanne akiwemo kaka yake, na baadaye kusamehewa na Rais John Magufuli Desemba 9, mwaka huu, amesema anajivunia kupata msamaha huo wa Rais wakati ambapo amefanikiwa kupata manufaa mbalimbali akiwa jela.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Pekos ambaye kipindi anapatwa na mkasa huo mwaka 1974 alikuwa mtoto wa miaka 12, anasema jela imeweza kumfundisha kusoma na kuandika, lakini pia imemfanya kuwa mbobezi katika ufundi wa kutengeneza sabuni.

Pekos na kaka yake wa tumbo moja, John Mtalikidonga (57), Yohana Chengula (71), Aloyce Mwalongo (80) na Raphael Mlyuka (75) walihukumiwa katika kesi ya mauaji ya mkazi wa mjini Njombe mwenye asili ya Kiasia (jina limehifadhiwa), iliyosikilizwa kuanzia mwaka 1974 na hukumu kutolewa mwaka 1978.

Alisema akiwa hajui kusoma wala kuandika kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 12, alitumwa na mama yake kutoka Kijiji cha Kifanya kwenda Njombe Mjini kwa kaka yake kwa ajili ya kuchukua fedha za matumizi na ndipo alipokutana na mkasa huo. “Nikiwa sijui hili wala lile nilijikuta mikononi mwa polisi, na baada ya siku mbili nikapelekwa mahakamani ambapo huko nikakutana na kaka yangu na wenzake watatu na kisha kusomewa mashitaka hayo ya mauaji,” alisema.

Katika hukumu ya awali ya Machi 14, 1978, Mahakama iliamuru Pekos na Mlyuka kufungwa kifungo cha miaka 10 gerezani huku kaka yake na Chengula wakihukumiwa kunyongwa. Alisema lakini baadaye mwaka 1980 ilitoka hukumu nyingine, iliyowaunganisha wote kwa pamoja kutumikia adhabu ya kunyongwa.

Alisema: “Pamoja na hayo yote sikuacha kumuomba Mungu kwani niliamini kuwa kila jaribu lenye mlango wa kuingilia, basi huwa halikosi mlango wa kutokea huku siku hadi siku nikijifunza namna ya kuishi vyema na wafungwa wenzangu kwa usimamizi wa askari Magereza, ambapo kutokana na umri wangu wengi walinichukulia kama mdogo wao.” Alisema moyo wake ulianza kupata matumaini mwaka 1983 baada ya Rais wa Awamu ya Kwanza Mwalimu Julius Nyerere kubatilisha adhabu ya kunyongwa na kuwa kifungo cha maisha gerezani, kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 21.

Alisema katika kipindi chote hicho, alitumikia hukumu yake katika magereza mbalimbali yakiwemo ya Iringa, Morogoro, Dodoma na Ukonga alipokuwa akitumikia hadi Desemba 9, mwaka huu walipoachiwa huru kwa msamaha wa Rais Magufuli.

“Alivyoingia madarakani Rais Magufuli, moyo ulizidi kujawa imani...kwa sababu kipindi chote nikiwa gerezani niliona na kusoma habari zake za upendo na huruma kwa wananchi wake, hivyo nami nilimuomba Mungu ajawe na hali ya imani ili kifungo chetu nacho kiweze kumgusa.

“Na ndiyo maana nasema siwezi kujisikia huru kama sitapata fursa ya kuonana naye ili niweze kumshukuru kwa moyo wa upendo alionao, kwa bahati nzuri Mungu anafanya kazi na yupo ndani ya moyo wake, naamini Mungu alimuambia kuwa inatosha sisi kuendelea kusota gerezani,” alisema Pekos. Akizungumzia msamaha wa Rais wa hivi karibuni, Pekos alisema anashukuru kuwa huru na kuepukana na mateso ya jela.

Aidha, alisema kwa kuwa sasa amerejea uraiani anatarajia kurudi kijijini (Kifanya) kukutana na ndugu zake, akiwemo kaka yake waliyekuwa wakitumikia adhabu moja, ila yeye akiwa amefungwa katika Gereza la Isanga Dodoma baada ya kutenganishwa mwaka 1979.

“Nashukuru Mungu nimetoka gerezani nikiwa najua kusoma na kuandika, niliingia nikiwa sijui kabisa kusoma wala kuandika kwa kuwa sikuwa nasoma shule kabla kutokana na hali mbaya ya uchumi aliyokuwa nayo mama yangu. “Lakini nafurahi pia nimetoka jela nikiwa nimejifunza kazi mbalimbali ikiwemo kilimo na utengenezaji wa sabuni, fani ninazotamani sana kuziendeleza kama nitawezeshwa kufanya hivyo,” alisema.

Alisema ni hamu yake kukutana na Rais Magufuli au Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage ili aweze kuwamegea maarifa ya mbinu za kuanzisha viwanda vidogo vya sabuni ili kuunga mkono jitihada za kuifanya Tanzania ya viwanda. “Tangu nikiwa jela nilikuwa namfuatilia kwa karibu Rais wangu, nafahamu jitihada zinazofanyika kuelekea Tanzania ya viwanda.

“Nami naunga mkono suala la ujenzi wa viwanda, nitapenda kumuunga mkono na kulipa fadhila ya utu huu alioufanya kwetu kwa kuanzisha kiwanda changu kidogo cha sabuni na pia kuwafundisha wenzangu utaalamu niliobobea nikiwa jela wa kutengeneza sabuni,” alisema Pekos.

Akizungumzia suala la kuoa, alisema kwa sasa hana mpango huo, lakini akasema suala hilo litategemea na namna Mungu atakavyomjalia kumudu maisha ya uraiani. “Siwezi kusema kama nitaoa au hapana, kwanza kwa sasa kila mwanamke namuona kama mama yangu, hivyo itanichukua muda mrefu kidogo kabla ya kuamua nioe au hapana, kikubwa naomba uzima.”

Katika hatua nyingine, Pekos aliiomba serikali kumsimamia ili aweze kupata haki ya mashamba yaliyopo katika Kijiji cha Mungilanziro, ambayo ni urithi waliopewa na baba yao kabla ya wao kufungwa, ili waweze kupata haki yao hiyo ya mashamba.

HABARI LEO

No comments: