ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 20, 2017

MBUNGE WA VUNJO NA MWENYEKITI NCCR MAGEUZI, JAMES MBATIA AMEPATA AJALI USIKU WA JANA NA KUVUNJIKA MKONO.

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi baada ya kuvunjika mkono.
Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), amevunjika mkono wa kushoto baada ya kuteleza na kuanguka na amelazwa katika wodi za watu mashuhuri (VIP).
Msaidizi wa mbunge huyo, Hamis Hamis amesema leo Jumatano Desemba 20,2017 kuwa tukio hilo lilitokea jana saa 2:45 usiku wakati akiondoka hotelini kurejea nyumbani.
Hamis amesema Mbatia alikuwa akishuka ngazi katika hoteli ya Uhuru iliyopo eneo la Shanty Town ndipo alipoteleza na kuanguka.
“Bahati nzuri pale kulikuwa na daktari wa KCMC anaiwa Ansbert Sweetbert ndiye alitoa huduma ya kwanza hadi kumpeleka KCMC,” amesema.
Amesema, “Kwa kweli huyo daktari alikuwa msaada mkubwa. Ndiye aliyempeleka KCMC na alikaa naye hadi saa nane usiku. Wauguzi na madaktari KCMC walimpa msaada mkubwa.”
Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi alipotafutwa leo mchana amesema bado maumivu aliyonayo ni makali kutokana na kuvunjika mkono.
“Bado nina maumivu makali. Nashukuru sana Mungu na jopo la madaktari limeshakutana na watafanya uamuzi,” amesema.
Mbatia amesema alishapatiwa matibabu ya mwanzo baada ya vipimo vya X-Ray kuthibitisha amevunjika mkono, lakini madaktari wanafanya tathmini ni huduma gani zaidi apewe.

Chanzo: Mwananchi

No comments: