ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 20, 2017

WATU SABA WAFARIKI KWENYE AJALI YA BASI NA HIACE MKOANI KIGOMA

Watu saba wamekufa papohapo na wengine 12 kujeruhiwa vibaya baada ya basi la kampuni ya Saratoga kugongana uso kwa uso na gari ndogo la abiria leo asubuhi mkoani Kigoma.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma, Sweetbert Njewike ameiambia MCL digital kwamba ajali hiyo imetokea leo saa 4:30 asubuhi katika kijiji cha Kabeba, kata ya Mwakizega katika wilaya ya Uvinza mkoani hapa huku akitaja uzembe wa madereva wote wawili ndio chanzo cha ajali hiyo.
Alimtaja dereva wa gari dogo Hassan ambaye pia ni mmiliki wa gari hilo kwamba ni miongoni mwa watu waliokufa huku dereva wa basi Bosco akishikiliwa na Polisi mjini Kigoma.
Alisema majeruhi wamelazwa katika kituo cha afya Ilagala na wengine wamekimbizwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Kigoma, Maweni kwa ajili ya matibabu zaidi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kabeba, Bakari Sungura ameiambia MCL Digital kwa njia ya simu kwamba haijawahi kutokea ajali ya aina hiyo katika historia ya kijiji hicho.
Amesema gari hizo zimegongana mita chache kutoka kwenye daraja ambapo gari hiyo ndogo iliburuzwa na kutupwa kwenye korongo chini ya daraja.

Chanzo: Mwananchi

No comments: