Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia wasichana wawili kwa kosa la kujihusisha na upangaji njama wa wizi wa pikipiki.
Wakati akizungumza na wanahabari jana Disemba 22, 2017 jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Kanda hiyo, SACP Lazro Mambosasa alisema wasichana hao wanaofahamika kwa majina ya Fatuma Jumanne (19) na Nasra Bakari (19), hutumika kama chambo kukodisha pikipiki kisha kuzipeleka kwa wakabaji.
“Watuhumiwa hawa walikamatwa baada ya askari kupokea taarifa ya tukio la unyang’anyi huko Ukonga Mazizini ambapo Mussa Hosea dereva wa bodaboda alikodiwa na wasichana hao kwa lengo la kuwapeleka mazizini, na wakati wanatoa pesa walijitokeza vijana watatu na kumkaba dereva wa pikipiki na kisha kutoroka nayo huku wasichana hao wakitoroka eneo hilo katika mazingira yasiyo eleweka,” alisema.
SACP Mambosasa alisema polisi walipowahoji wasichana hao, walionyesha nyumba ilikofichwa pikipiki hiyo, huko Ukonga Mazizini kwa Kapteni Mstaafu wa JWTZ Egno Paul (66).
Katika tukio lingine, SACP Mambosasa amesema mnamo Novemba 11 mwaka huu maeneo ya Vijibweni na Mbagala Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwakamata walinzi watatu wa kampuni ya Supreme International Guard waliokuwa zamu siku ya tukio la wizi wa mashine ya boti HP 85 Yamaha mali ya Wizara ya Mifugo na uvuvi yenye thamani ya milioni 18, iliyokuwa imeegeshwa kwenye ofisi ya TAFICO Kigamboni.
“Watuhumiwa hao baada ya kuhojiwa walikiri kuhusika na tukio hilo na kwamba mashine hiyo wameiuza Ilala kwa Bwana Katanga kwa bei ya Tsh milioni 2.5. Katanga alipokamatwa alieleza kuwa boti hiyo imesafirishwa kwenda Kigoma na ndipo yakafanyika mawasiliano na mashine hiyo kurudishwa jijini Dar es Salaam,” amesema.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni, Ramadhan Omary (41), Mohamed Abdallah (40), Rahis Faiya (29) na Mikidadi Hussein (40). Amesema upelelezi kwa watuhumiwa wote unaendelea na ukimalizika watapelekwa mahakamani kwa hatua za kisheria zaidi.
No comments:
Post a Comment