Advertisements

Thursday, December 28, 2017

UJENZI WA CHUO CHA VETA MKOA WA SIMIYU KUANZA MWEZI MACHI 2018


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa. Joyce Ndalichako(kulia) akiweka Jiwe la Msingi katika Mabweni ya Wasichana yaliyojengwa kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (P4R) katika Shule ya Sekondari Itilima wilayani Itilima Mkoa wa Simiyu,(kushoto) Mkuu wa Mkoa huo, mhe Anthony Mtaka.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa. Joyce Ndalichako akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lagangabilili mara baada ya kufungua vyumba vya madarasa vilivyojengwa kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (P4R) katika Shule ya msingi Lagangabilili wilayani Itilima Mkoa wa Simiyu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa. Joyce Ndalichako( wa tatu kushoto) na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Itilima na Mkoa wa Simiyu wakielekea kukagua vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Lagangabili, wakati wa ziara yake mkoani humo.

Na Stella Kalinga, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa. Joyce Ndalichako amesema Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi(VETA) cha Mkoa wa Simiyu kuanzia mwezi Machi, 2018.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara yake ya siku moja Mkoani humo.“Kesho tarehe 28/12/2017 kwenye magazeti kutatoka tangazo la zabuni ya ujenzi wa VETA ya Mkoa wa Simiyu na tunategemea kujenga VETA ya Kisasa itakayohudumia Mkoa na inayoendana na mahitaji ya sasa; tukitangaza zabuni kesho itachukua siku 30 kupokea zabuni unahitajika mwezi mmoja kufanya tathmini, nawaahidi kuwa ujenzi utaanza mwezi Machi” alifafanua Profesa Ndalichako.

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inasisitiza juu ya ujenzi wa Uchumi wa Viwanda inatambua umuhimu wa Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi ndiyo maana imejipanga kujenga vyuo hivyo pamoja na kuimarisha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.Aidha, Profesa Ndalichako amepongeza ongezeko la wanafunzi walioandikishwa kuanza darasa la kwanza na akasisitiza kuwa Wizara ya Elimu ambayo ndiyo inayotunga Sera itahakikisha inasimamia kikamilifu ili wanafunzi wote wanaoanza darasa la kwanza wamalize masoma yao.

Amesema ongezeko hilo ambalo limesababishwa na mwamko chanya wa wazazi baada ya kuanza kutekelezwa kwa mpango wa elimu bila malipo limepelekea upungufu wa miundombinu shule na ndiyo maana Serikali kuu inashirikiana na Halmashauri pamoja na wananchi katika ujenzi wa miundombinu ili kukabiliana na upungufu kupitia Mradi wa Lipa kulingana na Matokeo(P4R).

“Kupitia mradi wa Lipa kulingana na Matokeo tumeshajenga jumla ya vyumba vya madarasa 1104, matundu ya vyoo 3396, mabweni 261. Tunaendelea pia kuimarisha miundombinu katika sekta ya elimu kwa ujumla, kwa maana ya ukarabati katika vyuo vya Ualimu ambapo tumeshakarabati vyuo 17 na shule kongwe 46 kati ya shule 88 zimeshakarabatiwa” alisema Waziri.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa. Joyce Ndalichako(kushoto) akipokea maelezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi (kulia) wakati akikagua vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Lagangabili, wakati wa ziara yake mkoani Simiyu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa. Joyce Ndalichako(aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Itilima na Mkoa wa Simiyu mara baada ya kukagua vyumba vya madarasa vilivyojengwa kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo(P4R) katika Shule ya Sekondari Lagangabilili wilayani Itilima.

No comments: