Advertisements

Thursday, December 28, 2017

UKAGUZI MACHIMBO YA BUHEMBA KUKAMILIKA KABLA JANUARI 10, 2018

 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) mara baada ya kuwasili kwenye eneo la machimbo ya Dhahabu la Buhemba. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi.
 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa tatu kutoka kushoto) akikagua moja ya shimo la dhahabu kwenye machimbo ya Buhemba.
 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akijadiliana jambo na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi wakati wa ziara yake kwenye eneo la machimbo ya dhahabu la Buhemba, Wilayani Butiama, Mkoani Mara.
 Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi (aliyesimama) akimkaribisha Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) kuzungumza na Wachimbaji (hawapo pichani). Kushoto ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini (FEMATA), John Bina.
 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na baadhi ya Wachimbaji kwenye Machimbo ya Dhahabu ya Buhemba
Baadhi ya Wachimbaji kwenye Machimbo ya Dhahabu ya Buhemba wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani).


Serikali imeagiza kufikia Januari 10, 2018 Ukaguzi wa Usalama kwenye eneo la Machimbo ya Dhahabu ya Buhemba, Wilayani Butiama Mkoani Mara uwe umekamilika ili shughuli za uchimbaji zilizokuwa zimesimamishwa ziruhusiwe.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alitoa agizo hilo Desemba 27, 2017 alipofanya ziara kwenye eneo hilo ili kujionea hali halisi ya machimbo husika pamoja na kuzungumza na wachimbaji waliosimamishwa kuendeleza shughuli zao hadi hapo ukaguzi utakapokamilika. 
“Ninasikitika kuona shughuli za uchumi kwenye eneo hili la Buhemba zimesimama kutokana na shughuli za uchimbaji kusimamishwa baada ya kutokea ajali,” alisema. 
Serikali ilisitisha shughuli za uchimbaji Madini kwenye eneo hilo la Buhemba Februari 2017 baada ya kutokea vifo vya wachimbaji Watatu na wengine wapatao 15 kujeruhiwa kutokana na kufanya shughuli zao bila kuzingatia taratibu na kanuni za uchimbaji salama. 
Nyongo alisisitiza kwamba mgodi huo hautofunguliwa hadi hapo zoezi la ukaguzi litakapokamilika. “Hatuwezi kuufungua mgodi huu leo hii bila kukamilisha zoezi la ukaguzi kwahiyo kabla ya Tarehe 10 mwezi ujao, Wakaguzi wawe wamekamilisha ili mgodi uanze kazi na shughuli za uchumi zilizokuwa zikifanyika mgodini hapa zirejee,” alisema.
Alisema shughuli hiyo ya Ukaguzi inapaswa kukamilika mapema ili maduara yasiyo salama yaweze kutambulika na yazuiwe na yaliyokuwa salama yafahamike na kuendelezwa. 
Nyongo alikumbushia agizo alilotoa kwa Wakaguzi wa Migodi Desemba 14, 2017 Mkoani Tabora alipotembelea kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Nsungwa Gold Mine uliopo katika Kata ya Silambo Wilaya ya Kaliua la kukagua hali ya usalama na kuwasaidia Wachimbaji kuepusha ajali wakati wa utekelezaji wa shughuli zao.
“Ninawaagiza kwa mara nyingine Wakaguzi wa Migodi kuhakikisha mnatembelea maeneo ya migodi mara kwa mara ili kuepusha ajali,” aliagiza Naibu Waziri.

AIDHA, kwa upande mwingine, Naibu Waziri Nyongo amewataka Wachimbaji wa Madini kote nchini kutambua wajibu wao wa kulipa Tozo na Kodi mbalimbali Serikalini kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Alisema Serikali haina kikwazo na wachimbaji wadogo na inafanya jitihada za kuwasaidia kuwa na uchimbaji wenye tija hata hivyo alisema wanapaswa kutambua wajibu wao wa kulipa kodi ambayo itawanufaisha wao kama wachimbaji lakini pia Jamii inayozunguka maeneo yenye migodi na Taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa Rasilimali Madini ni kwa ajili ya Watanzania wote na kwamba kila Mwananchi anayo haki ya kunufaika nayo kwa namna moja ama nyingine mojawapo ikiwa ni manufaa yatokanayo na kodi zinazolipwa kutokana na shughuli za uchimbaji.
“Serikali inahitaji ipate kodi yake kwani madini yanapaswa kuwaneemesha Watanzania wote. Mtakavyolipa kodi, fedha husika zitatumika kuwaletea na kuwaboreshea huduma mbalimbali ikiwemo elimu, afya na miundombinu mbalimbali,” alibainisha Naibu Waziri Nyongo.
Aliongeza kuwa lengo la Serikali ni kuwarasimisha  Wachimbaji wa Madini kwa kuwapatia Leseni za Uchimbaji ili wachimbe kwa kufuata utaratibu unaotakiwa kama inavyoelekezwa kwenye Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017.
Naibu Waziri Nyongo yupo Mkoani Mara kwa ziara ya siku mbili ya kukagua shughuli za uchimbaji wa madini kwenye maeneo mbalimbali yenye migodi pamoja na kuzungumza na wachimbaji ili kubaini changamoto zinazowakabili kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi.

No comments: