Advertisements

Friday, December 29, 2017

Yanga yapata udhamini mpya

By GIFT MACHA

HUENDA zile shida ndogondogo zikapungua pale Jangwani kwa sasa baada ya mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, Yanga kuwa katika hatua za mwisho za kusaini mkataba mnono na kampuni ya vifaa ya Macron kutoka Italia.

Yanga ambayo ina mataji 27 ya Ligi Kuu kibindoni tayari imefanya mazungumzo ya awali na kampuni hiyo na huenda ikasaini mkataba huo mapema wiki ijayo.

Macron tayari imesaini mkataba wa miaka miwili na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambapo watakuwa wakitoa vifaa kwa timu zote za Taifa. Macron pia itawapa TFF Sh400 milioni kila mwaka kwa miaka yote miwili ya mkataba.

Licha ya kwamba Yanga inafanya siri, Mwanaspoti imepenyezewa taarifa kuwa nyota wa zamani wa timu hiyo, Aaron Nyanda ambaye yupo kwenye Kamati ya Masoko ya timu hiyo ndiye anayesimamia dili hilo. Nyanda ambaye ni Ofisa Masoko wa TFF, ndiye aliyekamilisha pia dili la Macron na shirikisho hilo.

Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba Yanga itasaini mkataba wa miaka miwili na Macron ambapo pamoja na mambo mengine, itapewa dola 250,000 (Sh556 milioni) kila mwaka.

Mbali na hivyo, Yanga itakuwa ikipokea mgawo wa faida kutokana na mauzo ya jezi zake kutoka kwenye kampuni hiyo, hivyo kila mwezi inaweza kuvuta kiasi kinachofikia Sh90 milioni.

“Dili linaweza kukamilika ndani ya siku tano ama sita zijazo. Dili lote linasimamiwa na Aaron Nyanda ambaye ndiye amefanikisha hao jamaa kusaini pale TFF, si unajua yupo kwenye Kamati ya Masoko ya Yanga, hivyo anawasaidia,” alisema mtoa habari huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Yanga kwa sasa ina udhamini wa SportPesa inayoipa Sh950 milioni kwa msimu huu, Azam TV wanaowapa Sh272 milioni pamoja na Maji ya Afya ambao wanawapa maji ya bure mazoezini na katika mechi.

Mkwanja huo huenda ukamaliza ukata uliopo klabuni hapo kwa sasa ikiwemo tatizo la kuchelewa kwa mishahara.

Pia, Yanga huenda sasa ikapata fedha za kuwalipa nyota wake wanaoidai klabu hiyo kama Beno Kakolanya aliyejitoa na Obrey Chirwa ambaye amegoma kurejea nchini, wote wakishinikiza kulipwa haki zao za kimkataba.

MWANASPOTI

No comments: