Advertisements

Monday, January 1, 2018

ASKOFU MKUU WA KANISA LA METHODISTI NCHINI AFARIKI

Askofu Mkuu wa kanisa la Methodisti nchini, Dk. Mathew Byamungu, amefariki ghafla usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Taarifa iliyotolewa na katibu wa kanisa la Methodisti, Askofu, Yusuf Bundala, ambaye pia ni askofu wa jimbo la Dodoma, imeeleza kuwa alipelekwa hospitali ya Muhimbili akitokea TMJ baada ya kujisikia vibaya kutokana na maradhi ya kisukari ambao alikuwa akisumbuliwa nao kwa muda mrefu na kufariki kabla ya kuanza kupatiwa matibabu.
Mipango ya mazishi inaendelea kufanyika katika kanisa kuu la Methodisti la Msasani mkabala na Shoppers plaza atazikwa Januari 4,2018 katika eneo la Kanisa la Methodisti la Boko.
Marehemu Byamungu alizaliwa mwaka 1954 mkoani kagera , alipata elimu ya msingi katika shule ya Kazilanfuka, sekondari (Kahororo na Mkwawa) , mafunzo ya ualimu katika chuo cha Chang’ombe jijini Dar es Salaam na baada ya kuhitimu alifundisha katika sekondari ya Azania jijini Dar es Salaam.
Kati ya mwaka 1981-1984 alijiunga na Chuo Kikuu cha Asia Centre for Theological na kupata shahada ya kwanza ya Theolojia na baada ya kuhitimu alirudi nchini na kufanya kazi ya uinjilishaji katika shule za sekondari na vyuoni jijini Dar es Salaam.
Mnamo mwaka 1987-1989 alikuwa Mchungaji wa kanisa la KKKT ambapo alitoa huduma katika makanisa ya Tabata na Mburahati na akiwa mchungaji wa kanisa hilo alianzisha kituo cha watoto yatima cha Calvary Cross Christian Centre -eneo la Boko jijini Dar es Salaam.
Mnamo mwaka 1990-1991 alisoma shahada ya pili ya Theolojia katika chuo kikuu cha Hyup Sung. Mnamo mwaka 2009 alitunikiwa Shahada ya Udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Latin California cha Marekani.
Mwaka 1991 alisimikwa kuwa mchungaji wa kanisa la Immanuel Methodist la nchini Korea na alipangiwa kuja kufanya kazi ya uinjilishaji nchini Tanzania, kazi ambayo aliifanya kwa ufanisi mkubwa na kufanikiwa kulisajili tawi la kanisa hilo nchini na kulibadilisha jina kutoka jina la awali la Tanzania Christian Methodist Church (TCMC) kuwa Tanzania Methodist Church (TMC) na kuongeza idadi ya waumini na makanisa ya Methodisti katika kipindi cha muda mfupi.
Mnamo mwaka 2003 alisimikwa kuwa askofu wa kwanza wa kanisa hilo nchini nafasi aliyoendelea kuitumikia hadi mwaka 2009 alipoteuliwa kuwa askofu Mkuu nafasi aliyokuwa nayo hadi kifo chake. Ameacha mke Jae-Young Ryu,ambaye pia ni Mchungaji Kiongozi na watoto wawili
Dk. Bya Mungu ataendelea kukumbukwa kwa kuasisi kanisa la Methodisti nchini na kuliendeleza ambapo chini ya uongozi wake limeweza kukua na kuwa na makanisa zaidi ya 30 nchini pia kanisa linashiriki kutoa mchango wa kuendeleza huduma za jamii kupitia sekta ya elimu na afya ambapo linaendesha shule na vituo vya afya na imekuwa ni kituo cha huduma ya mtoto (Compassion).
Mbali na kufanya jitihada kubwa za kuendeleza kanisa la Methodisti nchini, Askofu Bya Mungu aliona kuna umuhimu wa kuwa na viongozi wa kanisa wenye elimu na weredi ambapo chini ya uongozi wake kanisa lilianzisha chuo cha kutoa elimu kwa wachungaji na watumishi wa kanisa hilo kilichopo mjini Arusha , Alikuwa ni mhubiri wa kimataifa ambaye amefanya mahubiri katika nchi mbalimbali duniani na ameweza kuliunganisha kanisa na wadau mbalimbali ikiwemo serikali na taasisi mbalimbali za kimataifa za kidini na zisizo za kidini.
Marehemu katika uhai wake amekuwa ni kiongozi mnyenyekevu, muadilifu mwenye upendo na ushirikiano kwa watu wa ngazi zote. Ameacha ushuhuda na mfano wa Kuigwa.
Tunamuinua Mungu na Kumrudishia utukufu kwa zawadi aliyotupatia kwa muda tulioishi naye.

No comments: