ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 26, 2018

BALOZI SEIF AZITAKA ZAWA NA ZECO KUTIMIZA MAJUKUMU YAO



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akifanya ziara ya kukagua shughuli za maendeleo na kuona changamoto zinazowakabili Wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe.
Balozi Seif akisalimiana na Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Mwanakwerekwe “C” wakati akiwa katika ziara ya kuangalia shughuli za Maendeleo ndani ya Jimbo la Mwanakwerekwe.
Balozi Seif akiupongeza Uongozi wa Jimbo la Mwanakwerekwe kwa hatua yake ya kujenga Kituo cha Kazi ya Wahasiriamali kwa Vijana wa Jimbo hilo. Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmound na Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe Mh. Abdullah Ali Kombo.

Baadhi ya Wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe wakiwa katika Ukumbi wa Mikutano wa Meli Nne Saccoc kutoa changamoto zao kwenye Mkutano wa Majumuisho wa Ziara ya Balozi Seif.

Balozi Seif akizungumza na Wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe katika Mkutano wa majumuisho ya ziara yake hapo Meli Nne Saccoc.

                                                                                       Picha na – OMPR – ZNZ.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema changamoto nyingi zinazowakumba Wananchi katika maeneo yao zinaweza kupungua au kuondoka kabisa iwapo Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA}, Shirika la Umeme Zanzibar {ZECO} wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa kushirikiana na Mabaraza ya Mjini na Halmashauri za Wilaya Nchini.


Alisema uhaba wa huduma za Umeme na Maji Safi na Salama katika baadhi ya Mitaa Mjini na Vijijini umekuwa ukiwasumbuwa sana Wananchi hasa akina Mama na kupelekea kutumia muda wao mwingi kusaka huduma hizo badala ya nguvu zao kuzielekeza katika miradi ya Maendeleo.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika muendelezo wa ziara zake alizoziandaa Maalum za kutembelea Majimbo mbali mbali Nchini akiwa katika Jimbo la Mwnakwerekwe kujionea Mwenyewe Maendeleo na Changamoto zinazowakabili Wananchi katika Majimbo hayo.

Balozi Seif akikikagua Kituo cha Maji hapo Mwanakwerekwe “C” ambacho Transfoma yake kwa sasa imezidiwa matumizi na kuleta usumbufu wa upatikanaji wa Huduma za Maji sambamba na Umeme katika eneo hilo alisema ushirikiano wa pamoja ndio jambo la msingi linaloweza kuibua hitilafu zzinazojitokeza na nguvu hizo hizo zikatumika kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.

Alisema Mamlaka ya Maji Zanzibar na Shirika la Umme Zanzibar licha ya kupewa jukumu la kuhudumia Wananchi katika Sekta za Maji na Umeme lakini pia Taasisi hizo zinaweza kufanikiwa kukusanya mapato zaidi kama zitajenga mazingira bora zaidi ya Miundombinu hasa katika Miji yenye ongezeko kubwa la Watu.

Mapema Meneja Uendeshaji wa Shirika la Umeme Zanzibar Nd. Haji Silima alisema kutokana na usumbufu unaowakumbwa Wananchi wa Maeneo ya kwerekwe na juhudi za Viongozi wao wa kulitafutia ufumbuzi tatizo la umeme mdogo ZECO imeanza na hatua za awali za ujenzi wa njia mpya za kupitishia Umeme kuel;ekea kwenye Transfoma ya Mwanakwerekwe “C”.

Nd. Haji alisema mradi huo unaotarajiwa kugharimu jumla ya Shilingi Milioni 70,000,000/- zitakazotolewa na Shirika lenyenye pamoja na Mchango wa Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi “B” na Jimbo la Mwanakwerekwe utasaidia kuondosha tatizo la Umeme katika eneo hilo pamoja na upande wa Mitaa ya Tomondo.

Meneja huyo Muendeshaji wa ZECO alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba kazi hiyo iliyochelewa kumalizika kutokana na uhaba wa Vifaa pamoja na Fedha utakamilika Rasmi Mnamo Tarehe 10 Febuari Mwaka huu.

Naye Mwakilishi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} Nd. Maulid Khamis alimuhakikishia Balozi Seif kwamba miundombinu ya marekebisho ya mtandao wa Huduma za Maji safi na Salama katika eneo hilo kwa iko vizuri.

Nd. Maulidi alisema Fedha za mradi huo zimeshatengwa zinazofikia zaidi ya Shilingi Milioni 14,000,000/- na kinachosubiriwa kwa sasa ni ufungwaji wa Transfoma Kubwa Mpya katika Kisima hicho ili huduma za Maji safi irejee kama kawaida.

Balozi Seif katika ziara hiyo alikagua eneo lililotengwa na Baraza la Manispaa la Wilaya ya Magharibi “B” kwa ajili ya Maegesho ya Gari za Abiria zinazokwenda na kurudi njia ya Wilaya ya Kusini Unguja hapo uwanja wa Jitimai ya zamani Magogoni.

Kituo hicho kimelenga kuondosha msongamano katika eneo la Mwanakwerekwe pamoja na soko lake ambapo Gari za Abiria zitalazimika kukaa zamu katika kituo hicho mkapa itapofika wakati wake kwa ajili ya kutoa huduma za usarifi kwa abiria.

Balozi Seif alimalizia ziara yake kwa kuangalia Jengo kubwa la Kisasa lililojengwa na Uongozi wa Jimbo la Mwanakwerekwe kuwa Kituo cha Wajasiriamali cha Vijana wa Jimbo hilo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Jimbo la Mwanakwerekwe chini ya Mwakilishi wake Mh. Abdulla Ali Kombo kwa juhudi iliyochukuwa ya ujenzi wa Kituo hicho utakaopunguza wimbi la Vijana wasiokuwa na ajira ambao hupelekea kufanya vitendo vilivyo nje ya maadili.

Akizungumza katika majumuisho ya ziara hiyo baada ya kupokea changamoto mbali mbali zinazowakabili Wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe hapo Ukumbi wa Meli Nne Saccos Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alionya kwamba Kiongozi asiyekubali kujikita katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015/2020 atalazimika kuangaliwa kwa Tahadhari na Viongozi wa Kitaifa.

Balozi Seif alisema Chama cha Mapinduzi kilitangaza Ilani na Sera zake kwa wananchi ilipokuwa ikiomba ridhaa ya kuongoza Dolan a kufanikiwa kupewa jukumu hilo. Hivyo Viongozi wake hawatokubali kuona baadhi ya watendaji wa Taasisi za Umma Serikalini wanaichezea Ilani hiyo kwa kuwadhihaki Wananchi.

Kuhusu uvamizi wa maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa kazi maalum kana Kilimo na miradi ya huduma za Jamii Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kutahadharia Jamii kwamba Serikali italazimika kuchukuwa maamuzi magumu wakati wa Utekelezaji wa Ripoti ya Kamati iliyoundwa kufanya utafiti wa maeneo hatarishi.

Alisema Wilaya mbili za Magharibi “A” na “B” zilizomo ndani ya Mkoa Mjini Magharibi ndizo zinazokuwa Muhanga wakati wa Msimu wa Mvuza za Masika zinazosababisha mafuriko kutokana na Ujenzi holela unaofanywa na baadhi ya Watu Wasiozingatia taratibu za ujenzi.

Akigusia vitendo vya Ubakari vinavyooneka kufuru ada Balozi Seif alitahadharisha wazi kwamba hakutakuwa na hatua zozote zitakazochukuliwa na vyombo vya Kisheria iwapo Wananchi watashindwa kufika Mahakami kutoa ushahidi pale wanapotakiwa kufanya hivyo.

Alisema Kesi zinazotokana na vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia zinazoripotiwa kila kukicha hivi sasa zimeshapindukia zaidi ya 200 hali inayolitia aibu Taifa katika uso wa Dunia.

Mapema akitoa ufafanuzi wa changamoto zilizowasilishwa na Wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshima Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Serikali kupitia Mradi wa Huduma za Mijamii Mijini {ZUSP} inaangalia uwezekano wa kuinyanyua zaidi Bara bara Kuu itokayo Mwanakwerekwe kuelekea Makaburini.

Hatua hiyo ambayo kwa sasa iko katika hatua za utafiti na uchambuzi imekuja kutokana na eneo hilo kukumbwa na mafuriko wakati wa Mvua za Masika na hatimae kusababisha usumbufu wa usafiri kwa Wananchi na hata wageni wanaotumia Bara bara hiyo kwa shughuli za Kiutalii.

Alisema haipendezi kuona Bara bara hiyo hujaa Maji na kutuwama katika Bwawa la Mwanakwerekwe kutokana na mafuriko ya Mvua na kuzuia shughuli zote za usafiri.

Akiitolea ufafanuzi changamoto ya Gari za Ng’ombe na Punda zinazochafua mazingira katika Shehia ya Mwanakwerekwe Mkuu huyo wa Mkoa Mjini Magharibi amewahahkikisha Wananchi hao kwamba zoezi la kuondosha mifugo hiyo litakamilika ndani ya Wikio Moja.

Mh. Ayoub aliwataka Wananchi kushirikiana na Serikali ya Mkoa chini ya Kamati ya Ulinzi katika kuhakikisha kadhia hiyo inayowatia hofu Wananchi inaondoka mara moja kutokana na wahusika wa mifugo hiyo kutumia silaha za jadi wakati wa kujihami. 

No comments: