Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akiwasili kijiji cha Hoteli Tatu, Kata ya Mandawa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi kwa ajili ya kuembelea kampuni ya Universal Mining Ltd kujionea hali ya uzalishaji wa jasi (Gypsum) unavyoendelea wakati wa ziara ya Siku tatu katika Mkoa wa Lindi na Mtwara, Leo 17 Januari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akikagua uzalishaji wa madini aina ya Jasi (Gypusm) katika kijiji cha Hoteli Tatu, Kata ya Mandawa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, Leo 17 Januari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akizungumzia umuhimu wa wachimbaji wadogo kuwa na umoja ili kukuza ufanisi na tija katika kupanga bei ya rasilimali wanazozalisha wakati alipozuru kijiji cha Hoteli Tatu, Kata ya Mandawa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, Leo 17 Januari 2018.
Na Mathias Canal, Lindi
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko Leo 17 Januari 2018 amewataka wachimbaji wadogo wa madini Jasi(Gypsum) kuwa na umoja na mshikamano katika uuzaji madini hayo na kuwa na kauli moja katika ushiriki wa soko la bidhaa hiyo.
Mhe Biteko ameyasema hayo alipotembelea katika kijiji cha Hoteli Tatu, Kata ya Mandawa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi wakati wa ziara ya Siku tatu katika Mkoa wa Lindi na Mtwara ambapo pamoja na mambo mengine atakutana na makundi ya wachimbaji wadogo ili kubaini changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Alisema kuwa kila mchimbaji anajipangia gharama aitakayo yeye pasina kushirikiana na wachimbaji wengine ili kuwa na bei moja ambayo itakuwa na tija na manufaa kwa kila mmoja hivyo kupitia umoja wao watakuwa na kauli na maamuzi ya pamoja yenye tija na faida kwao.
Mhe Biteko aliwashauri wachimbaji hao kuwa na umoja utakaokuwa na uwezo wa kudai bei itakayofanana kwa wote pia kuwa na uwezo wa kutengeneza sheria ndogondogo ambazo zitatumika kujisimamia wao wenyewe.
Aidha, amezitaja Changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi sambamba na wachimbaji wadogo hususani ubovu wa barabara ambapo ameishauri Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kusaidia utengenezaji wa Barabara itakayorahisisha usafirishaji wa jasi (Gypusm) na kurahisisha huduma za wananchi ili kufika kwa urahisi katika Barabara kuu.
Mhe Biteko alisema kuwa serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli itaendelea na juhudi zake za kuweka miundombinu rafiki kwa ajili ya wananchi, wawekezaji, na wachimbaji (wakubwa na wadogo) hivyo ili kufikia adhma ya mafanikio hayo ni lazima kusema na kutekeleza maelekezo yote ili kupiga hatua za maendeleo.
Alibainisha kuwa nia ya sekta ya madini ni kufanya mchakato wa kuongeza pato la Taifa kufikia asilimia 10% tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo sekta ya madini inachangia kiasi kidogo kwenye pato la Taifa.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment