NA TIGANYA VINCENT
VIONGOZI wa vyama
vya ushirika vya msingi (AMCOS) wameagizwa kuhakikisha
wanasimamia wanachama wao wanapanda miti ili kuhifadhi mazingira na
kupata nishati ya kukaushia tumbaku.
Kauli hiyo ilitolewa jana wilayani
Urambo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akitangaza wiki ya
upandaji miti kwa ngazi ya AMCOS na wanachama wake.
Alisema kuwa kama wahitaji wa kuni
za kukaushia tumbaku yao wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanaungana na Serikali
kutumia miundo mbinu walionayo kuhakikisha wanapanda miti katika maeneo na
mashamba yoa ili zao hilo liwe endelevu.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa
Kampuni zinazonunua tumbaku mkoani humo zimekuwa zikiwapa wakulima miche za
miti lakini baadhi ya Vyama vya Ushirika Vya Msingi vimekuwa vikiishia katika
kuitupa chini ya miti mikubwa au vingine kuiacha katika Ofisi za vyama husika.
Mwanri alisema kuwa Ushirika ni
chombo chenye nguvu na hivyo wakitumia nafasi walionayo watasaidia sana katika
zoezi la upandaji miti mkoani Tabora kwa ajili ya kugeuza Tabora kuwa ya kijani
na kuongeza kiwango cha mvua.
Alisema kuwa ili kuhakikisha kuwa
wakulima hao wameitikia wito huo wataendesha zoezi la ukaguzi wa mashamba ya
wakulima wa tumbaku ya miti na ya Ushirika yaliyopandwa mwaka huu ili
kujiridhisha kama wametekeleza agizo hilo.
Naye Afisa Ushirika kutoka Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Fortunatus Mkoba aliwakumbusha wanaushirika kuwa
wanatakiwa kila mkulima kuhakikisha kuwa anapanda miti 250 kwa kila ekari moja
ya tumbaku anayopanda kila mwaka.
Alisema kuwa utaratibu huo upo
Kisheria na Mkulima asiyetekeleza jukumu hilo hapaswi kulima tumbaku.
Mkoba aliwataka viongozi wa AMCOS
kuhakikisha wanawahimiza wanachama wao kutekeleza matakwa hayo ya kisheria
kwani kinyume cha hapo ni uvunjaji wa Sheria na viongozi ambao watashindwa
kuwasimamia wanachama wa watachukuliwa hatua.
Aliongeza kuwa bila miti hakuna
tumbaku , hivyo ni vema wakaitikia wito wa viongozi ili waweze kuendelea kulima
zao hilo ambalo ni zao kuu la biashara kwao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Adam Malunkwi alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Tabora
kuwachukulia hatua wakulima wa tumbaku ambao wamekuwa wakivunja Sheria ya
kuwataka kupanda miti 250 kabla ya kulima ili iwe fundisho kwa wengine.
Alisema kuwa hatua ikichukuliwa kwa
wale wanaopuuzia basi itakuwa fundisho kwa wengi kutii na kuanza kupanda miti.
No comments:
Post a Comment