ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 10, 2018

WANANCHI WA LIWALE NA NACHINGWEA WALILIA BARABARA

 Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akionesha Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa watendaji wa Wilaya ya Liwale (hawapo pichani), ambapo utekelezaji wa miradi yote ya barabara hapa nchini umeanishwa humo wakati alipowatembelea kuona hali ya mtandao wa barabara katika wilaya hiyo, mkoani Lindi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Sara Chiwamba.
 Mkuu wa Wilaya ya Liwale mkoani Lindi, Bi. Sara Chiwamba akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, kuhusu haAli ya mtandao wa barabara wilayani humo katika ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo, mkoani humo kukagua miundombinu hiyo.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Bi. Rukia Muwango kuhusu nia ya Serikali ya kuhakikisha inafungua wilaya hiyo na wilaya jirani ya Liwale kwa kuwajengea barabara kwa kiwango cha lami, mkoani Lindi.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akisisitiza jambo kwa uongozi wa Wilaya ya Ruangwa wakati alipofanya kikao nao wilayani hapo. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Joseph Mkirikiti.
 Muonekano wa sehemu ya barabara ya Ruangwa- Namichiga KM 22 ambapo Wakala wa Barabara mkoa wa Lindi wamepewa jukumu la kuhakikisha inapitika wakati wote.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi Mzawa kutoka Kampuni ya Southern Link, Mhandisi Felix Aminieli, anayejenga Daraja la Nandanga lenye urefu wa mita 30 ambalo lipo katika mto wa Lukuledi, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi. Kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw.Joseph Mkirikiti.
 Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Lindi, Mhandisi Isaack Mwanawima akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua za ujenzi wa daraja la Nandanga lenye urefu wa mita 30 ambalo lipo katika mto wa Lukuledi, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Muonekano wa daraja la Nandanga ambalo lipo katika barabara ya Wilaya ya Luchelegwa-Ndanda inayounganisha wilaya za Ruangwa mkoa wa Lindi na Masasi mkoani Mtwara. Daraja hilo linatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu.

Wananchi wa wilaya ya Liwale na Nachingwea mkoani Lindi wameiomba Serikali kuhakikisha inaanza ujenzi wa barabara ya Liwale - Nachingwea (Km 129) kwa kiwango cha lami ili kutatua changamoto za usafirishaji wa abiria na mazao katika wilaya hizo. 
Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, Mkuu wa wilaya ya Liwale Bi. Sarah Chiwamba amesema kuwa wanachi wake wanaamini kuwa Liwale itafunguka kibiashara na kiuchumi endapo itakuwa imeimarishwa katika mtandao wa barabara ambazo zitaiunganisha wilaya hiyo na wilaya jirani pamoja na nchi kwa ujumla.

"Naamini barabara hizi zikikamilika wilaya hii na mkoa wetu utaendelea kiuchumi kwani suala la miundombinu ya barabara imekuwa ni kilio cha muda mrefu katika wilaya yetu", amesema Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Bi. Sarah amefafanua kuwa wananchi wengi katika wilaya hiyo ni wakulima, hivyo wamekuwa wakitumia miundombinu ya barabara kusafirisha mazao ya korosho na ufuta yanayozalishwa kwa wingi kuelekea maeneo mbalimbali ya nchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri huyo anayeshughulikia masuala ya Ujenzi, amewataka wataalamu wote wa masuala ya ujenzi nchini kupitia Sera ya Ujenzi ya mwaka 2003 ambayo itawasaidia kuwapa mwongozo katika utekelezaji wa majukumu yao katika kutoa huduma bora kwa jamii.

Ameongeza kwa wataalam wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kuwa wabunifu katika ujenzi wa barabara zao ili kuondoa dhana potofu iliyopo dhidi ya usimamizi wa barabara kati yao na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

"TANROADS na TARURA shirikianeni katika kuhakikisha mnawajengea wananchi miundombinu iliyobora, kusiwepo na utofauti kati ya barabara mnazozisimamia", amesema Naibu Waziri huyo.

Ametoa wito kwa uongozi wa TANROADS mkoani Lindi kuhakikisha kuwa wanaboresha maeneo yote ya barabara ambayo ni korofi ili yaweze kupita kiurahisi katika kipindi chote cha mwaka. 
Naye, Meneja wa TANROADS mkoani Lindi, Mhandisi Isaack Mwanawima, amemhakikisha Naibu Waziri Kwandikwa kuendelea na mpango wa matengenezo ya barabara kwa kiwango cha lami ili kufungua fursa mbalimbali katika mkoa huo.
Naibu Waziri Kwandikwa yupo katika ziara ya kikazi mkoani Lindi kujionea hali halisi ya mtandao wa barabara katika mkoa huo ambapo pamoja na mambo mengine ametembelea na kukagua daraja la Nandanga lenye urefu wa mita 30 ambalo lipo kwenye mto Lukuledi katika barabara ya wilaya ya Luchelegwa- Ndanda inayounganisha wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi na Masasi mkoa wa Mtwara ili kujionea miundombinu yake.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments: