Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akipanda kiberenge kwenda kukagua ukarabati wa reli iliyoharibika kwa mvua katika eneo la umbali wa kilomita mia moja lililopo kati ya Kilosa, Morogoro na Gulwe, Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Bwana Masanja Kaodogosa (wa pili kulia) akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia) kazi ya kukarabati reli ikiendelea unaofanywa na wafanyakazi wa Shirika hilo baada ya kuharibika kwa mvua wakati wa ziara yake ya kukagua ukarabati huo katika kijiji cha Mkadage kilichopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akishuka kwenye tingatinga inayojaza udongo kwenye eneo lililopo katika kijiji cha Munisagala kilichopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro baada ya kukagua kazi inayoendelea ya kujenga na kurejesha miundombinu ya reli iliyoharibika na mvua wakati wa ziara yake kwenye eneo hilo. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Bwana Masanja Kadogosa.
Kazi ya kujaza udongo kwenye eneo la ukubwa wa mita 170 lililopo katika kijiji cha Munisagala kilichopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro ikiendelea kwa ajili ya kujenga na kurejesha miundombinu ya reli iliyoharibika na mvua.
Mhandisi Mkuu Ujenzi
wa TRL Mhandisi Nelson Ntejo akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano (kulia) uharibifu wa miundombinu ya reli uliotokea kutokana na mvua
wakati wa ziara yake ya kukagua uharibifu huo na ukarabati unaoendelea kati ya
Kilosa, Morogoro na Gulwe, Dodoma. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Reli Tanzania Bwana Masanja Kadogosa.
Serikali imetoa miezi
sita kwa wananchi wanaolima ndani ya eneo la hifadhi ya reli inayopita Wilaya
ya Kilosa mkoani Morogoro kuhama eneo hilo baada ya kuvuna mazao yao ili
kuhifadhi miundombinu ya reli na kupunguza uharibifu wa miundombinu hiyo.
Hayo yameelezwa na
Naibu Waziri wa uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ua Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara yake alipotembelea
kukagua ukarabati wa reli iliyopo eneo la Kilosa, Morogoro na Gulwe, Dodoma
lenye umbali wa kilomita mia moja baada ya kuharibika kwa mvua na Serikali
kusitisha usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa
mbali mbali na nchi za jirani.
Nditiye amesema kuwa
uharibifu wa eneo hilo ni wa kiwango kikubwa kwa kuwa katika kipande cha umbali
wa kilomita mia moja zilizoharibika kwa mvua baadhi ya maeneo reli imebomoka,
kuhama kwenye njia yake na ardhi husika kuliwa na maji ya mvua yaliyojaa kwenye
mto Mkondoa ambao unapita pembezoni mwa reli hiyo.
Ameongeza kuwa
uharibifu huo unasababishwa na shughuli za kibinadamu ambapo wananchi wanaishi
na kulima ndani ya mita thelathini upande wa kulia na kushoto mwa reli ambapo
ni hifadhi ya miundombinu ya reli na wananchi hawaruhusiwi kutumia eneo hilo
kwa shughuli yeyote. “Nakuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania
Bwana Masanja Kadogosa ushirikiane na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa kuwahamisha
wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi hii wakishavuna mazao yao kwa kuwa kilimo
kinasababisha mmomonyoko wa udongo hivyo kuharibu miundombinu ya reli”,
amesisitiza Mhandisi Nditiye.
Amesema kuwa Wizara
yake itawasiliana na kushirikiana na Wizara ya Maji, Kilimo na Umwagiliaji ili
waweze kukarabati mabwawa makubwa matatu ya Hombolo, Kidete na Manyara ili
yaweze kuhifadhi maji na kuyadhibiti kama ilivyokuwa hapo awali ili
yasipitilize kuingia kwenye mto huo bila kufunguliwa kwa utaratibu na kuharibu miundombinu ya reli.
Naye Mkurugenzi Mkuu
wa Shirika la Reli Tanzania Bwana Masanja Kadogosa amesema kuwa tayari Shirika
lake limeleta vifaa na wafanyakazi katika eneo hilo ambapo wanafanyakazi kazi
mchana na usiku ili kuhakikisha kuwa reli hiyo inaanza kutumika tena kwa
shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo.
Ameongeza kuwa kwa siku Shirika
lake linapoteza takribani shilingi milioni mia mbili ambazo ni chanzo cha
mapato kwa Shirika hilo na Serikali kwa ujumla. Amesema kuwa Shirika lake
limefanya tathmini na kubaini kuwa kiwango cha uharibifu wa reli hiyo ni
kikubwa na tayari ameiomba Serikali impatie jumla ya shilingi million 994 za
kukarabati eneo hilo.
Aidha, Bwana Kadogosa
amewashukuru wakandarasi wanaojenga reli mpya ya kisasa ya SGR kwa kuwa
wazalendo na kuwapatia vifaa ambavyo wanavitumia kukarabati eneo hilo. Mmoja wa
wafanyakazi wa Shirika hilo akiwa katika moja ya eneo la tukio lililopo katika
kijiji cha Mkadage wilayani Kilosa mkoani Morogoro, akizungumza kwa niaba ya
wafanyakazi wenzake, Bwana Jumanne Kinyasi ameiomba Serikali kumpatia Bwana
Kadogosa fedha hizo na kuwaongeza vifaa ili waweze kukarabati reli hiyo ili
waweze kurejesha huduma kwa wananchi.
Bwana Kadogosa amemweleza Mhandisi
Nditiye kuwa ukarabati huo utakamalika mapema wiki ya pili ya mwezi Januari
mwaka huu. Bwana Kadogosa
alifafanua kuwa reli hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto ya kuharibika kila
baada ya kipindi cha miaka kumi ambapo iliwahi kuharibika tena mwaka 1998, 2007
na sasa mwaka huu 2018 kutokana na mabadiliko ya majira ya mvua, tabia nchi na
hali ya hewa. Ameongeza kuwa Serikali inaendelea na mazungumzo na wafadhili wa
kutoka Japan na mkandarasi anayejenga reli ya kisasa ili kuweza kupata
mwarobaini wa kudumu wa kudhibiti na kuondoa kabisa uharibifu wa miundombinu ya
reli hiyo.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment