Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi wa Ujerumani nchini, Dkt. Detlef Wachter pamoja na ujumbe alioongozana nao.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akiagana na mgeni wake Balozi wa Ujerumani nchini, Dkt. Detlef Wachter mara baada ya mazungumzo yao jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Kamwelwe amekutana na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Dkt. Detlef Wachter na kuzungumzia ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika kuinua kiwango cha huduma ya maji na usafi wa mazingira nchini. Katika kikao hicho kilichofanyika Ofisi za Wizara ya Maji na Umwagiliaji jijini Dar es Salaam, kililenga kuimarisha uhusiano mzuri wa Serikali hizo mbili kwa lengo kukuza maendeleo ya Sekta za Maji, ambapo Ujerumani imeendelea kuwa mdau wake mkubwa.
Mhandisi Kamwelwe ameishukuru sana Ujerumani kwa mchango wake mkubwa ambao imekua ikiutoa na kukiri umekuwa na manufaa makubwa sana kwa Tanzania, akitolea mfano utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji ya Sumbawanga, mkoani Rukwa ambao umekamilika na Kigoma ambao uko katika hatua za mwisho kukamilika kwa ufadhili wa Serikali ya Ujerumani. Pia, Waziri Kamwelwe amesema Tanzania inategemea kutekeleza miradi mikubwa sita nchini kwa ufadhili wa Ujerumani na kuwakaribisha wawekezaji zaidi kutoka Ujerumani kwa ajili ya kuwekeza kwenye Sekta za Maji na Umwagiliaji.
Aidha, Balozi wa Ujerumani nchini, Dkt. Wachter amesema Sekta ya Maji ni moja ya sekta inayopewa kipaumbele katika ushirikiano huo na kumuhakikishia Waziri Kamwelwe dhamira ya Ujerumani kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuinua kiwango cha huduma ya maji na usafi wa mazingira nchini .
No comments:
Post a Comment