Mkurugenzi
Mtendaji wa Kiwanda cha Sunflag cha mjini Arusha, Ajay Shah, akiongoza
zoezi la kuchoma nyavu haramu za dagaa zilizo chini ya sentimita
8 (marobota 584) zenye jumla ya shilingi milioni mia moja zilizokamatwa
kwenye Kiwanda chake na Kikosi Kazi Maalum cha Kutokomeza Uvuvi Haramu
nchini kilichoundwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga
Joelson Mpina kwenye dampo la takataka nje kidogo ya jiji la Arusha
leo.(Na John Mapepele)
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Joelson Mpina (mwenye kofia) akikagua
chumba cha baridi cha kuhifadhia samaki (Cold room) cha kampuni ya Alpha
Choice mjini Arusha leo akiwa katika operesheni maalumu
ya kudhibiti uvuvi haramu kulia ni mmliki wa kampuni hiyo Yussuf Khatry.
(Na John Mapepele)
Marobota
584 ya nyavu haramu yaliyotengenezwa na Kiwanda cha Sunflag cha mjini
Arusha yenye thamani ya shilingi milioni 100 wakitekea kwenye dampo
nje ya jiji la Arusha leo. Marobota hayo alikamatwa na Kikosi Kazi Maalum
cha Kutokomeza Uvuvi Haramu nchini kilichoundwa na Waziri wa Mifugo
na Uvuvi, Mhe. Luhaga Joelson Mpina ambapo uteketezaji huo uliongozwa
na mmliki wa kiwanda hicho Ajey Shah(Na John
Mapepele)
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Joelson Mpina (mwenye kofia) akisikiliza
taarifa ya ukamataji wa marobota 584 ya nyavu haramu yaliyotengenezwa
na Kiwanda cha Sunflag cha mjini Arusha yenye thamani ya shilingi milioni
100 kutoka kwa kiongozi wa Kikosi Kazi Maalum cha Kutokomeza Uvuvi
Haramu nchini West Mbembati aliye kulia, kushoto mwakilishi wa
Afisa Tawala wa Mkoa wa Arusha David Lyamongi. (Na John
Mapepele)
- Mmiliki wa kiwanda aongoza zoezi la kuteketeza nyavu zilizokamatwa kwenye kiwanda chake.
Na John Mapepele
Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina amekitoza faini ya Shilingi milioni
mia moja Kiwanda cha Sunflag Tanzania Limited cha jijini Arusha
baada ya kukutwa na makosa mawili ambayo ni kuzalisha na kuuza
nyavu bila kuwa na leseni kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kuzalisha
na kuuza nyavu ambazo ziko kinyume na matakwa ya Sheria ya Uvuvi
namba 22 ya mwaka 2009.
Kulingana na maelezo
ya Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Ajay Shah, kiwanda kimekuwa
kikitengeneza vyavu hizo haramu kwa miaka mitatu mfululizo sasa
ambapo inakadiliwa kuwa tayari kimeshatengeneza tani 1296 nyavu
hizo zenye thamani ya shilingi bilioni nne.
Akitoa taarifa kwa Waziri
Mpina, Kiongozi wa kikosi kazi cha kutokomeza uvuvi haramu katika
kanda ya Ziwa Victoria, West Mbembati amesema kuwa tarehe 17/1/2018
walifika kwenye kiwanda hicho na kukamata marobota 584 yenye thamani
ya milioni mia kufuatia maelekezo ya Waziri Mpina yaliyotolewa
Mjini mwanza hivi karibuni baada ya mfanyabiashara Dastan Venanti kukamatwa
na nyavu hizo zenye thamani ya milioni sitini na tano ambazo nyaraka
zilionyesha alinunua katika kiwanda hicho.
Akipokea taarifa hiyo
Waziri Mpina alisema mkakati uliopo kwa sasa ni kuwabaini watengenezaji
na wasambazaji wote wa zana haribifu za uvuvi ikiwa ni pamoja na vyavu
zisizoruhusiwa kisheria ambapo amesema hatua za kali za kisheria dhidi
yao zitatumika ili kudhibiti uvuvi haramu kwenye maji(mito,maziwa
na bahari) ya nchi yetu.
“Operesheni ya kuwabaini
na kuwachukulia hatua wafanya biashara wakuu wanaofadhili na kuendeleza
biashara ya uvuvi haramu ni ya kudumu ambapo mkakati uliopo sasa
ni kuwanyang’anya na kuwafutia lesseni zao za biashara” alisisitiza
Mpina
Aliwaonya wafanyabiashara
wanaosafirisha samaki na mazao yake katika nchi za jirani za Uganda,
Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kongo wanaotishia kugoma ambapo amesisitiza
kwamba hatua waliyoichukuwa ni ndogo badala yake waachane kabisa na
biashara hiyo kwa kuwa wamekuwa wakikwepa kodi na kuikosesha Serikali
mapato yake kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa Kiwanda hicho, Ajay Shah alikiri kutenda makosa hayo na
kueleza kuwa kiwanda kimekuwa kikiendelea kutengeneza vyavu hizo
bila kujua kuwa kilikuwa hakizingatii sheria za Uvuvi ambapo
alisema kimekuwa kinauza nje ya nchi hususan kwenye soko la Nairobi
nchini Kenya na Mwanza
Aliwataja baadhi ya
wateja wake wakuu wa mkoani Mwanza kuwa ni pamoja na Dastan Venant,
Morice Otieno na Majani Masagati ambao wote walikamatwa hivi karibuni
na nyavu zisizoruhusiwa kisheria na kikosi kazi cha kudhibiti
uvuvi haramu kilichoundwa na Waziri Mpina na kutozwa faini ya jumla
ya shilingi milioni 120 huku vyavu hizo zikitaifishwa na kuteketezwa
mara moja.
Katika hatua nyingine
Mkurugenzi huyo aliongoza zoezi la kuteketeza nyavu hizo haramu
kwa kushirikiana na Waziri na Watendaji mbalimbali wa Serikali
katika dampo la kuwekea takataka nje kidogo ya jiji la Arusha huku akikiri
kuwa atazingatia taratibu zote za Serikali katika kutengeneza
nyavu zinazoruhusiwa kisheria ambapo alisema tayari wameshapeleka barua
Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kupata kibali cha kutengeneza
nyavu.
Aidha Waziri Mpina ametoa
siku tatu kwa Watendaji wa Wizara yake kumempatia kibali cha kutengeneza
nyavu hizo kwa mujibu wa sheria za nchi. Kulingana na Sheria ya Uvuvi
namba 22 ya Mwaka 2003 kibali hicho kinatolewa na Mkurugenzi wa Idara
ya Maendeleo ya Uvuvi.
1 comment:
Hapakuwa na namna nyingine ya kubadilisha matumizi ya nyavu hizo ,ili isiwe hasara kwa pande zote mbili serikali na mwekezaji?
Post a Comment