ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 4, 2018

WAZIRI MWAKYEMBE AUNDA KAMATI YA KUPITIA KATIBA YA MCHEZO WA NGUMI.

 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza leo Jijini Dar es Salaam na Wadau wa mchezo wa ngumi hapa nchini ambapo ameunda Kamati ya Watu kumi na moja watakaoandaa Katiba ya mchezo huo ndani ya mwezi huu. 
 Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini Bw. Yusuph Singo(aliyesimama) akizungumza leo Jijini Dar es Salaam na Wadau wa mchezo wa ngumi hapa nchini  kabla ya Mhe Waziri Mwakyembe wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kuuunda Kamati ya Watu kumi na moja watakaoandaa Katiba ya mchezo huo ndani ya mwezi huu.
 Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw. Mohamedi Kiganja akitoa muongozo wa kikao  baina ya Mhe.Waziri  Harrison Mwakyembe (aliyekaa katikati) na wadau wa ngumi nchini leo Jijini Dar es Salaam.
 Mwanamasumbwi wa zamani Bw.Yassin Ustadhi akichangia mawazo wakati wa kikao cha Mhe. Waziri Mwakyembe wa Wizara ya Habari  Utamaduni Sanaa na Michezo na wadau wa mchezo wa ngumi leo Jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja

Na Shamimu Nyaki-WHUSM
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe ameunda kamati ya watu kumi na moja watakaopitia Katiba ya kusimamia mchezo wa ngumi  za kulipwa hapa nchini pamoja na kukusanya maoni  namna bora ya kuendesha mchezo huo itakayoanza kazi  kuanzia Januari 03 hadi 31 ambapo  itakuwa chini ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) .

 Akizungumza na wadau wa mchezo huo Jijini Dar es Salaam Mhe.Waziri ameiagiza Kamati hiyo kufanya kazi kwa pamoja katika kuunda mfumo mpya utakaolinda maslahi ya mabondia na wahusika wote wa mchezo huo ili kuleta heshima ya mchezo huo hapa nchini.

“Naomba mshirikiane katika kazi hii vunjeni makundi yenu ili mfanye kazi kwa maslahi ya Taifa na wanamasumbwi wetu,mkifanya hivyo tutaleta hamasa kubwa kwa watu wengi kujiunga na mchezo huu ambao unaleta ajira kwa vijana wetu”.Alisema Mhe.Waziri Mwakyembe.

 Kamati hiyo itaongozwa na mwenyekiti Emmanueli Salehe ambaye ni mdau mkubwa wa ngumi hapa nchini,akisaidiwa na makamu Mwenyekiti Joe Enea ambaye ni Mwalimu wa ngumi pamoja na katibu Bw.Yahya Pori ambae pia ni mdau wa mchezo huo.

Wajumbe katika kamati hiyo ni Bw. Habibu A.Nyogoli mwanamasumbi wa zamani, Shomari Kimbau ambae ni muandaaji wa mapambano ya ngumi,Bw.Fike Wilson mwalimu wa ngumi,Bw.Anthony Ruta,mdau wa ngumi,Dkt.Killaga M.Killaga ambaye ni daktari wa wanamasumbwi hapa nchini.Wengine ni wanamasumbwi ambao ni Bw.Ally B Champion, Bw.Rashidi Matumla,na Bw.Karama Nyilawila ambao wameitangaza vyema nchi yetu katika mchezo huo.

Ameongeza kuwa katik kipindi hiki cha mpito shughuli za kutoa vibali kwa mapambano ya ndani na kwa mabondia wanaosafiri nje ya nchi zitaendelea kutekelezwa na BMTambapo  ameiagiza BMT kuendelea kusimamia vibali vya safari za nje za mabondia kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za nchi.

Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Michezo (BMT) Bw.Mohamed Kiganja ameihakikishia  kamati hiyo ushirikiano wa kutosha ili kutimiza adhma ya Serikali kuendeleza mchezo huo hapa nchini pamoja na kuwanufaisha wanamichezo hao.

Naye Bondia wa zamani Bw.Yassin Ustadh ameishukuru Serikali kwa kuamua kuunda Kamati hiyo ambapo amesema itaondoa migogoro mingi na ya muda mrefu iliyopo katika mchezo huo inayosababisha kupoteza hadhi yake na kutowanufaisha mabondia. 

No comments: