Advertisements

Thursday, February 1, 2018

KAMATI YA BUNGE YAOMBA MKATABA MLIMANI CITY KUCHUNGUZWA

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeliomba Bunge kumuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa mchakato wa mikataba yote ya mradi wa Mlimani City.
Akiwasilisha bungeni leo Februari1, 2018 taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka amesema kamati hiyo imebaini dosari katika mkataba wa uendeshaji wa mradi huo, kusababisha Serikali kukosa mapato.
Miongoni mwa dosari alizozitaja za mradi huo ni kukiukwa kwa sheria ya Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC) inayotaka ili kibali cha uwekezaji kutolewa lazima mwekezaji alete ushahidi kuwa na mtaji wa kutosha.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilikodisha eneo hilo kwa kampuni ya Mlimani Holding Ltd.
Hivi karibuni PAC ilifanya ziara katika eneo la Mlimani City na kuutaka uongozi wa UDSM kurekebisha mkataba kati yake na kampuni ya Mlimani City Holding Ltd kutokana na mapungufu yaliyojitokeza, huku ikihoji sababu ya mwekezaji huyo kuja na mtaji wa Sh150,000 tu.
Licha ya kutotaja siku, Kaboyoka amesema mara ukaguzi huo utakapokamilika taarifa yake iwasilishwe bungeni.

Chanzo: Mwananchi

No comments: