ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 26, 2018

MAKAMU WA RAIS APOKEA VIFAA MBALI MBALI VYA WALEMAVU KUTOKA SERIKALI YA KUWAIT

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia Vifaa vya Walemavu vilivyotolewa na Serikali ya Kuwait ,pichani ni Balozi wa Kuwait nchini Jasem Al Najem (katikati) na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi Ajira na Watu wenye Ulemavu, Stella Ikupa . (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akijaribu kusukuma kiti maalum cha magurudumu kwa ajili ya walemavu mara baada ya kukabidhiwa na Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Jasem Al Najem (kulia), wengine pichani ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi Ajira na Watu wenye Ulemavu, Stella Ikupa  na Msaidizi wa Balozi wa Kuwait nchini Bi. Zainab Ally.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa makabidhiano ya baadhi ya vifaa vya walemavu vilivyokabidhiwa na Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Jasem Al Najem, wengine pichani ni Msaidizi wa Balozi wa Kuwait Bi. Zainab Ally (kushoto) na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi Ajira na Watu wenye Ulemavu, Stella Ikupa . (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amepokea Vifaa vya Walemavu vyenye thamani ya dola za kimarekani elfu thelathini .

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo Makamu wa Rais alisema kuwa anaishukuru Serikali ya Kuwait kwa Misaada wanayotoa kwa Tanzania.

“Leo tumepata tena msaada kutoka Kuwait wa Vifaa vya Walemavu, tumepokea vigari vya walemavu vya aina tatu au nne tofauti, tumepokea vifaa vya Albino,vifaa vya wasioona kuanzia vya kuangalia kwa wale wenye uwezo mdogo mpaka vya kuandikia”

Makamu wa Rais alisema kuwa amezungumza na Balozi wa Kuwait nchini  kuhusu mahitaji ya visima vikubwa vya maji kwenye baadhi ya maeneo yenyeshida ya maji na ujenzi wa vituo vya upasuaji.

“Nimetoka kwenye ziara Iringa, Simiyu na nimekuta tatizo kubwa la maji, wananchi wanahitaji visima kwa wingi kwa hiyo nimeongea nae na ameonesha kukubali kuchimba visima virefu kwa yale maeneo yenye ukame”.

Kwa upande wake Balozi wa Kuwait Mhe. Jasem Al Najem alisema wanamshukuru Makamu wa Rais kwa kutenga wakati wake siku ya leo kwa ajili ya kupokea vifaa vitakavyosaidia ndugu zetu wenye ulemavu wa viungo na ngozi.

“Huu ni mpango kamili wa kuwasaidia walemavu wa viungo na ngozi ambao unafadhiliwa na Serikali ya Kuwait”

Aidha, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi Ajira na Watu wenye Ulemavu, Stella Ikupa alisema ubalozi wa Kuwait umekuwa ukifanya mambo mengi katika nchi yetu kwa watu wenye ulemavu na leo tumepokea vifaa vingi sana na tunawashukuru sana .

No comments: