Advertisements

Tuesday, February 27, 2018

Mbowe na vigogo Chadema waripoti Polisi Dar

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho wanakwenda kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mchana Jumatatu Februari 27, 2018 Mbowe amesema wanakwenda kuripoti kuitikia wito wa Polisi.
Amesema katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji hatakwenda kwa kuwa yupo nje ya nchi na atakaporejea atakwenda kwa kuwa hawana sababu ya kugoma.
Februari 20,2018 Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam iliagiza kukamatwa viongozi saba waandamizi wa Chadema akiwamo Mbowe.
Wito huo ulikuja siku chache baada ya tukio la kuuawa kwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.
Viongozi wengine mbali ya Mbowe na Dk Mashinji ni naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).
Pia, wamo mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee; mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche na Esther Matiko ambaye ni mweka hazina wa Bawacha.
Mdee, Matiko, Heche na Mnyika walisharipoti awali na walitakiwa kurejea kituoni leo. Viongozi wengine waliwakilishwa na wanasheria.
Mbowe akizungumza na waandishi wa habari amesema wana taarifa kuwa watakamatwa na kwamba kuna mpango wa kubambikiziwa kesi.

No comments: