ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 21, 2018

MVUA, UPEPO WALETA TAFRANI NAMTUMBO

NA  YEREMIAS  NGERANGERA
Upepo  mkali ulioambatana na mvua umeleta tafrani katika kijiji cha Njalamatata kata ya Mkongo Nakawale wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma .

Tafrani  hiyo ilitokea siku ya  jumatatu  wiki hii  baada ya nyumba tano kuezuliwa na upepo na wananchi waliokumbwa na dhahama hiyo kubaki wakitafuta makadhi  ya kujihifadhi kwa majirani.

Katibu tawala wa wilaya ya Namtumbo bwana Adelin Nchimbi akiwa na kamati ya ulinzi na usalama  walifika eneo la tukio na kuongea na  waathirika wa tukio la kuezuliwa nyumba katika  kijiji cha Njalamatata.

Aidha bwana Nchimbi alisema kuwa katika tukio hilo Nyumba tano ziliezuliwa na  upepo  lakini   hapakujitokeza  mwananchi yoyote kujeruhiwa au kuwepo kwa  maafa katika tukio hilo.

Alitaja majina ya wananchi walioathirika katika tukio hilo ni  Clavery Ponera ,Donatus Kapinga,James Mdagi ,Sadiki Kapinga ,Rusti  Kimbili na Lotary Hongo wote ni wakazi wa kijiji hicho cha Njalamatata wilayani humo.
 Kamati  ya ulinzi na usalama  ya wilaya ya Namtumbo pamoja  na kutoa pole kwa waathirika wa tukio hilo ilifanya mahojiano na waathirika kubaini hasara iliyopatikana  kutokana na tukio hilo.
Kamati ya ulinzi  na usalama ya wilaya ya Namtumbo pamoja na pole hizo iliwashauri wananchi wa kijiji hicho kujenga nyumba na kuziezeka kwa kuweka tengo za kushikizia kwenye ukuta baada ya kubaini baadhi ya nyumba hazikuwekwa tengo hizo.

No comments: