Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (kulia) akizungumza na Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa Bwana Ajuaye Msese wakisafiri kwa boti ndani ya ziwa hilo kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na uchukuzi kwenye mwambao wa ziwa hilo. Aliyevaa miwani ni Meneja Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mhandisi Albert Richard
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akikagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na uchukuzi mkoani Rukwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo. Aliyeshika simu ni Mwenyekiti wa CCM mkoani humo Bwana Reina Lukala
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mwalimu Julieth Binyula akimuonesha Meneja Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mhandisi Albert Richard maeneo ambayo hayana mawasiliano wakiwa kwenye bandari ya Kasanga wilayani humo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na uchukuzi mkoani Rukwa
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (kushoto) akipata taarifa ya mkoa wa Rukwa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Joachim L. Wangapo wakati wa ziara ya yake ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na uchukuzi mkoani humo
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (kushoto) akisalimiana na Meneja wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) mkoa wa Rukwa Bwana Peter Kuguru alipowasili wakati wa ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na uchukuzi mkoani humo
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (akiwa ndani ya gari la kwanza) akitoka kwenye bandari ya Kasanga iliyopo ziwa Tanganyika wakati wa ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na uchukuzi mkoani Rukwa. Pembeni ni muonekano wa ziwa Tanganyika
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amefanya ziara ya kikazi ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwa wananchi waishio kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa na Tanganyika katika maeneo ya vijiji mbalimbali viliyopo kwenye mkoa wa Njombe, Mbeya na Rukwa.
Mhandisi Nditiye amefanya ziara hiyo ili kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi waishio kwenye mwambao huo ili kujiridhisha kuhusu uwepo wa huduma hizo ambapo Serikali kupitia Wizara hiyo inaipatia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ruzuku inayoziwezesha kampuni za simu za mkononi kufikisha huduma za mawasiliano vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.
Katika ziara hiyo, Mhandisi Nditiye amebaini uwepo wa mawasiliano hafifu kwenye baadhi ya maeneo na mahali pengine hamna mawasiliano yoyote kwa wananchi waishio mwambao wa ziwa Nyasa na Tanganyika. “Nimesafiri kwa boti ndani ya ziwa Nyasa kutoka eneo la Lupingu, Ludewa mkoani Nyasa hadi matema mkoani Mbeya na sasa kwenye bandari hii ya Kabwe mkoani Rukwa, nimeshuhudia mwenyewe ukosefu wa mawasiliano ya uhakika kwa wananchi waishio kwenye mwambao wa ziwa ambapo lolote likitokea ukiwa ndani ya ziwa huwezi kabisa kuwasiliana,” amesema Mhandisi Nditiye.
Ameongeza kuwa Serikali inatambua unuhimu wa wananchi kuwasiliana kwa kuwa mawasiliano yanachangia ukuaji wa pato la wananchi na taifa kwa ujumla, yanawezesha na kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa eneo husika. Amesema kuwa tayari Wizara kupitia UCSAF imefanya tathmini ya kufikisha huduma za mawasiliano kwa kuzipatia ruzuku kampuni za simu za mkononi ili ziweze kujenga minara ya simu za mkononi.
Mhandisi Nditiye amefafanua kuwa ukosefu wa mawasiliano haimaanishi uwepo wa minara michache ya simu za mkononi ya kampuni fulani na ukosefu wa mnara wa kampuni mojawapo ya mawasiliano ya simu za mkononi, bali eneo ambapo hamna mnara wa simu za mkononi wa kampuni yoyote ile.
Ameongeza kuwa hadi hivi sasa Serikali imefikisha huduma za mawasiliano vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa kiwango cha asilimia 94, na ni maeneo machache tu ambayo yamebaki hayajafikiwa na huduma za mawasiliano. “Serikali imejipanga na kuhakikisha kuwa huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi waliosalia ifikapo mwaka 2020 ambapo wananchi waishio kwenye mwambao wa ziwa Nyasa na Tanganyika wamepewa kipaumbele hicho”, amesema Mhandisi Nditiye.
Akitoa maelezo yake kwa Mhandisi Nditiye kuhusu mpango huo wa Serikali wa kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi waishio kwenye mwambao, Meneja wa Uendeshaji wa UCSAF Mhandisi Albert Richard amesema kuwa, tayari Mfuko umeyabaini maeneo hayo, kufanya tathmini ya mahitaji ya minara na fedha husika ili kuweza kufikisha huduma za mawasiliano kwenye baadhi ya maeneo ya wananchi waishio kwenye mwambao wa maziwa hayo. “Tumetembea Ludewa kwenye Tarafa ya Mwambao yenye kata nne za Kilondo, Lumbila, Lupingu na Makonde zilizopo mwambao wa ziwa Nyasa na kubaini uwepo wa mawasiliano hafifu na mahali engine hakuna mawasiliano kabisa ambapo Serikali imetenga kiasi cha dola za marekani 252,500 ambazo zitatumika kufikisha mawasiliano”. Amesema Mhandisi Richard.
Akizungumza na Mhandisi Nditiye kuhusu hali ya mawasiliano na miundombinu mengine kwenye mkoa huo, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Mhe. Andrea Tsere amesema kuwa tayari Serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) inaendelea na kazi ya kupita kwenye eneo la mwambao wa ziwa Nyasa ili kuweza kujenga barabara kwa kuwa wananchi waishio eneo hili hawana barabara ya uhakika. Pia, amemshukuru Mhandisi Nditiye kwa kufanya ziara hiyo na kuzungumza na wananchi ambapo amewahakikishia kuwa Serikali inakamilisha ujenzi wa meli mpya kwa ajili ya eneo hilo na itajenga minara ya mawasiliano ili kutimiza ahadi ya Serikali ya Awamu ya Tano inaayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwatumikia wananchi.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Nditiye akiwa mkoani Rukwa kwenye bandari ya Kabwe na Kasanga na bandari ya Itungi, iliyopo Kyela mkoani Mbeya, amelielekeza Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari kufunga mitambo ya mawasiliano kwenye meli mpya ili abiria waweze kuwasiliana wakiwa ndani ya meli kwa kuwa wengine ni wafanyabiashara wanaosafirisha mizigo ndani na nje ya nchi kupitia maziwa hayo. Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya Bwana Godfrey Kawache amemueleza Mhandisi Nditiye kuwa kuna ukosefu wa mawasiliano kwenye baadhi ya maeneo ya kata ya Nguna, Ngonga, Busele, Kajungumele na maeneo ya Kandete na Ibada.
Mhandisi Nditiye aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mwalimu Julieth Binyula na wa Nkasi Bwana Said Mohamed Mtanda wa Mkoa wa Rukwa akiwa katika ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na uchukuzi katika maeneo ya mkoani Rukwa. Bwana Mtanda amemuomba Mhandisi Nditiye kuwaelekeza wataalamu wake kushirikiana na Ofisi za Wakuu wa Wilaya kutekeleza majukumu ya Serikali kwa manufaa ya wananchi.
No comments:
Post a Comment