ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 26, 2018

Polisi Dar wamdaka anayewalaghai wanawake

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limemkamata mkazi wa Kinondoni, Rajabu Mohamed (25) maarufu Rajeshi kwa tuhuma za kuwakamata wanawake, kuwaingiza kwa nguvu kwenye gari lake, kuwapora na kuwafanyia vitendo vya ukatili.
Akizungumza leo Februari 26, 2018, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa eneo la Kinondoni akituhumiwa kuwapata wanawake kwa kuwalaghai kuwa ni mfanyabiashara.
Amesema mtuhumiwa huyo baada ya kuwapora wanawake huzunguka nao katika gari na kuwatishia kuwa ni freemason na anaweza kuwaua kwa kuwanyonya damu au kuwakata maeneo mbalimbali ya miili yao.
“Kupitia vitisho hivyo wanawake walilazimika kutoa neno la siri la simu zao ambapo alichukua kadi zao za benki na kuwaibia fedha zao kupitia mashine za kutolea fedha (ATM),” amesema Mambosasa.
Amesema mbali na kuwabaka na kuwalawiti huwashusha na kuwatelekeza vichochoroni.
“Hadi sasa tumepokea kesi tatu na nilipomhoji aliniambia kuwa ni kweli alikuwa akifanya vitendo hivyo, lakini kwa sasa ameacha. Hatuwezi kuvumilia vitendo vyake. Upelelezi unaendelea ili kuwabaini wale wote anaoshirikiana nao,” amesema.

No comments: