ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 20, 2018

TRA yasema Kakobe anahifadhi fedha kwenye ndoo

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imebaini mambo matano baada ya kumchunguza Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Followship (FGBF), Zachary Kakobe, ikiwemo kukwepa kodi na kuhifadhi mabilioni ya fedha katika majaba na ndoo.
Taarifa iliyotolewa leo Februari 20 na Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Charles Kichere pia imesema Kakobe alimuandikia barua Rais John Magufuli kutokana na matamshi yake kwamba ana fedha nyingi kuliko Serikali, kumuomba radhi.
Mambo yaliyobainika baada ya kufanyika kwa uchunguzi huo
  1. Imesema Askofu huyo hana akaunti wala fedha katika taasisi ya fedha hapa nchini. Aidha uchunguzi ulibaini kuwa Askofu Kakobe ni mmoja wa wasimamizi wakuu wa akaunti za kanisa zilizopo katika benki ya NBC zenye jumla ya kiasi cha Sh8.2bilioni, kiasi hiki cha fedha kimetokana na sadaka, zaka na changizo ambazo zinatolewa na waumini wa kanisa tajwa hapo juu, hivyo kwa mujibu wa sheria hakitozwi kodi.
  2. Kanisa lilikwepa kulipa kodi kiasi cha Sh20.8milioni.
  3. Kampuni inayomilikiwa na watoto wa Askofu Kakobe ilikwepa kulipa kodi ya Sh37.2 ambazo zimelipwa baada ya uchunguzi. Kwa ujumla kiasi kilicholipwa kutokana na uchunguzi ni Sh58.1milioni.
  4. Kanisa linatunza kiasi kikubwa cha fedha kwenda ndoo na ‘majaba’ kinyume na taratibu za utunzaji fedha.
  5. Kanisa halitengenezi hesabu za mapato na matumizi ya fedha kitu ambacho ni kinyume na katiba ya kanisa na sheria ya usimamizi wa fedha ambayo imepelekea matumizi mabaya ya fedha za waumini kama vile safari za nje ya nchi ambazo zimedhaminiwa na kanisa lakini wanaosafiri ni Askofu na familia yake.

No comments: