Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiongea na kinamama walioshiriki kwenye Songambele ya Ujenzi wa upanuzi wa kituo cha Afya Kirando muda mfupi kabla ya kinamama hao kuruhusiwa na kuwaachia wanaume kuendelea na kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili kutoka kushoto) akipokezana na wananchi mawe ya msingi yanayojengewa msingi wa kituo cha afya cha kirando siku ya uzinduzi wa songambele ya upanuzi wa ujenzi wa kituo hicho.
Wanananchi wa Kirando waliojitokeza kushiriki katika Songambele ya ujenzi wa Kituo cha afya Kirando.
Wanananchi wa Kirando waliojitokeza kushiriki katika Songambele ya ujenzi wa Kituo cha afya Kirando.
Zaidi ya wananchi 1200 wa kata ya Kirando inayojumuisha vijiji vinne vya Mtakuja, Mpata, Kichangani na Kamwanda, Wilayani nkasi Mkoani Rukwa, wajitokeza katika kuhakikisha uchimbaji na uwekaji wa msingi wa kituo cha afya cha kirando unakamilika ili kuweza kuanza upanuzi na ujenzi wa kituo hicho kitakachohudumia kata zaidi ya nne katika tarafa ya Kirando.
Wananchi hao wamejitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi za Rais Dk. John Pombe Magufuli katika kuhakikisha huduma hizo za kiafya zinasogezwa karibu na wananchi yao ili kuokoa maisha ya kina mama wajawazito, watoto na wahitaji wengine wa huduma hizo ambao wanaishi karibu na kituo hicho na kuongeza kuwa umbali wa kutoka Kirando hadi hospitali ya Wilaya iliyopo Namanyere ni Kilometa 61.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo aliyeongoza harambee hiyo amesema kuwa wameamua kuungana na wananchi pamoja na kuwashirikisha ili kuwajulisha wananchi juhudi zinazofanya na wananchi na kuonyesha mshikamano kuwa maendeleo hayaji bila ya mshikamano.
“Kila mtu anaguswa na afya, mtoto, mzee na kijana wote, serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dk. John Pombe Magufuli imeamua kuboresha na kupanua vituo vya afya ili huduma zisogee karibu kuliko kutegemea hospitali za wilaya, kwa hali hiyo ndio maana serikali inapanua vituo vya afya ili tuupunguze msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali zetu pamoja na kwenye vijiji na tarafa huduma ziwe bora zaidi.” Alifafanua.
Miongoni mwa kinamama waliohudhuria katika Songamebele hiyo Hamisa Heri amesema “Tunamshukuru Mh. Magufuli kwa muda mrefu kumekuwa na shida ya huduma ya uzazi mapaka uende Namanyere ni mbali, mtu unakuwa na shida lakini hapa baadhi ya vifaa hakuna na kama alivyosema mkuu hapa kama vifaa hivyo vitapatikana maana yake vitatusaidia na hata wengine waliopo vijiji vinavyozunguka hapa, kituo hichi kitawasaidia.”
Nae binti aliyeshiriki katika songamebele hiyo Deliza Mngumenya ametoa shukurani zake kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha za upanuzi wa kituo hicho na kusogeza huduma bora karibu na wananchi ambapo ana uhakika kituo hicho kitakapokamilika wataweza kupata vipimo vyenye ufanisi.
Upanuzi wa kituo hicho utahusisha majengo manne ikiwemo jengo la Wazazi au mama na mtoto, Chumba cha Upasuaji, Maabara pamoja na Mochwari pamoja na vifaa vyake vitakayogharimu jumla ya shilingi milioni 700, kati ya hizo shilingi milioni 300 zitatumika kununulia vifaa.
No comments:
Post a Comment