Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza (wanne kushoto) akiangalia namna ambavyo mwanariadha mstaafu Filbert Bayi (kushoto) alivyoweka historia katika mashindano ya Jumuiya ya Madola miaka ya sabini wakati wa hafla iliyoandaliwa na Balozi wa Australia nchini Mhe. Alison Chartres (watatu kushoto) kuadhimisha ujio wa michezo ya jumuiya ya madola ya 21 jana Jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Australia nchini Tanzania Mhe. Alison Chartres akizungumza jana Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuadhimisha ujio wa michezo ya jumuiya ya madola ya 21 itakayofanyika nchini Australia Aprili mwaka huu.
Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza (katikati) akimpa mkono mchezaji wa timu ya mpira wa meza Bi. Neema Mwaisyula atakayeshiriki katika mashindano ya jumuiya ya madola mwaka huu jana wakati wa hafla fupi ya kuadhimisha ujio wa michezo ya jumuiya ya madola ya 21 yatakayofanyika nchini Australia mwezi Aprili mwaka huu. Kushoto ni Balozi wa Australia nchini Tanzania Mhe. Alison Chartres na kulia ni Mkurugenzi wa Michezo Bw. Yusuph Singo
Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza (kulia waliokaa) katika picha ya pamoja na wanamichezo kutoka Tanzania watakaoshiriki michuano ya jumuiya ya madola yanayotarajiwa kufanyika nchini Australia mwezi Aprili mwaka huu. Katikati waliokaa ni Balozi wa Australia nchini Tanzania Mhe. Alison ChartresPicha na: Genofeva Matemu - WHUSM
Na: Genofeva Matemu - WHUSM
Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza amewataka wanamichezo watakaoenda nchini Australia kushiriki mashindano ya jumuiya ya madola kutumia uwezo wao wa hali ya juu kwani wamepewa dhamana kubwa na nchi ya kupeperusha vyema bendera ya nchi katika mashindano hayo.
Rai hiyo ameitoa jana Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla iliyoandaliwa na Balozi wa Australia nchini kuadhimisha ujio wa michezo ya jumuiya ya madola ya 21 itakayofanyika mwezi Aprili katika mji wa Gold Coast nchini Australia.
Mhe. Shonza amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wanamichezo wote nchini na kuwataka washiriki wa mashindano ya jumuiya ya madola kutoka Tanzania kuenzi mazuri yaliyowahi kufanywa na wachezaji wenzao katika mashindano hayo ya jumuiya ya madola.
“Ni faraja kubwa sana kwetu kwa kukaribishwa na mwenyeji wetu wa Australia, nikuhakikishie tu kuwa wachezaji wetu wamejiandaa vizuri na watashiriki vizuri na hata kuchukua medali katika mashindano hayo” amesema Mhe. Shonza
Kwa upande wake Balozi wa Australia nchini Tanzania Mhe. Alison Chartres amesema kuwa kwa mara ya kwanza mashindano ya jumuiya ya madola yatakuwa na medali sawasawa kwa jinsia zote na hii itasaidia kuongeza usawa na adhi ya jamii ili kupunguza ubaguzi ndani ya jamii na kuweka uwiano sawa.
Aidha Mhe. Chartres amewatakia kila la heri wachezaji kutoka Tanzania watakaoshiriki mashindano ya jumuiya ya madola kwa kuiwakilisha nchi vizuri kwani kila anayeenda katika mashindano hayo tayari ni mshindi kwa namna moja hivyo wachezaji watumie nafasi walizopata kushiriki mashindano hayo kuiletea sifa nchi ya Tanzania.
Timu kutoka Tanzania zitakazoshiriki katika mashindano ya jumuiya ya madola yatakayofanyika mwezi Aprili mwaka huu nchini Australia katika mji wa Gold Coast ni pamoja na timu ya mchezo wa Riadha, Timu ya mchezo wa mpira wa meza, Timu ya mchezo wa ngumi, pamoja na Timu ya mchezo wa kuogelea.
No comments:
Post a Comment