ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 20, 2018

WAZIRI MKUU ATEMBELEA KIWANDA CHA NYAMA MISUNGWI

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitaza uchakataji wa nyama ya ng’omba wakati alipotembelea kiwanda cha nyama cha Tanbeef kinachomilikiwa na kampuni ya Chobo Investments Company katika eneo la usagara wilayani Misungwi Februari 19, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama nyama ya ng’ombe na mbuzi iliyofungashwa kitalaamu tayari kwa kuuzwa ndani na nje ya nchi wakati alipotembelea kiwanda cha nyama cha Tanbeef kinachomilikiwa na kampuni ya Chobo Investments Company katika eneo la usagara wilayani Misungwi Februari 19, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea na kukagua kiwanda cha kusindika nyama cha Kampuni ya Chobo Investment kilichpo wilayani Misungwi chenye uwezo wa kuchinja ng’ombe 600 mbuzi na kondoo 920 kwa siku.
Alitembelea kiwanda hicho kinachomilikiwa na wazawa jana (Jumatatu, Februari 19, 2018) wakati akiwa katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza. Alisema amefarijika na uwekezaji huo.

Alisema uwekezaji wa aina hiyo ulikuwa unasubiriwa sana nchini kwa sababu unakwenda kupunguza tatizo la wafugaji kutokuwa na soko la uhakika wa mifugo yao, hivyo Serikali itamuunga mkono ili kiwanda hicho kiwe endelevu.

Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza sera ya uchumi wa viwanda na inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika viwanda mbalimbali, ambapo aliipongeza kampuni hiyo kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda

Akizungumzia kuhusu changamoto ya kutokuwa na maeneo ya kunenepeshea na kulisha mifugo yao, Waziri Mkuu alisema tayari alishamuagiza Waziri wa Mifugo Bw. Luhaga Mpina kushughulikia suala hilo na kwamba litapatiwa ufumbuzi.

Pia Waziri Mkuu aliwataka watumishi waliojiriwa katika kiwanda hicho wafanye kazi kwa bidii, wawe waaminifu na waadilifu.

Awali, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Bw. John Chobo alisema kiwanda hicho kinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji, hivyo kinategemea maji ya kisima au ya kuletwa na boza kutoka Mwanza mjini jambo ambalo linachangia katika kuongeza gharama za uzalishaji.

Baada ya kutoa malalamiko hayo Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga  kushughulikia suala hilo na ahakikishe kiwanda hicho kinapata maji. Kiwanda hicho kipo umbali wa kilomita nne kutoka Ziwa Victoria.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya eneo la kulishia na kunenepeshea ng’ombe Bw. Chobo alisema kampuni yake iliomba kupatiwa eneo kutoka kwa Serikali tangu mwaka 2014 karibu na kiwanda hicho lakini hadi sasa hawajapatiwa.

Kiwanda hicho kinauza bidhaa zake ndani na nje ya nchi. Nchi hizo ni Oman, China, Canada na Misri. Baadhi ya wanunuzi hao kutoka Omani ni Bw. Tahir Al Hashim na kutoka China ni Bw. Kingsong Shao walisema nyama inayochakatwa kiwandani hapo ni nzuri na ina ubora wa kimataifa.

Pia kiwanda hicho kinasambaza nyama katika migodi yote mikubwa nchini ambayo awali ilikuwa inaagiza nyama kutoka nje ya nchi, hivyo, Mkurugenzi wa kiwanda hicho aliiomba Serikali kuwasaidia katika kulinda soko la ndani.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMANNE, FEBRUARI 20, 2018.

No comments: