JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA YA UFAFANUZI KUHUSU RAIA WA TANZANIA NCHINI OMAN
Kuna
kipande cha video kinasambaa mitandaoni kikiwa na maelezo kuwa raia wa Tanzania
wanaoishi nchini Oman wamekusanyika ofisi ya Ubalozi kushinikiza kurejeshwa
nyumbani kutokana na mateso na adhabu kali wanazopata kutoka kwa mabosi wao.
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, baada ya kutazama kipande
hicho cha video iliwasiliana na Ubalozi wa Tanzania nchini Oman kwa madhumuni
ya kujua usahihi wa jambo hilo.
Ubalozi
ulitoa ufafanuzi kuwa uliandaa mkutano wa Watanzania wote wanaoishi Oman na
ulipangwa kufanyika katika hoteli ya Golden Tulip jijini Muscat tarehe 23 Machi
2018. Matangazo ya mkutano huo yalitaka Watanzania watakaopenda kushiriki
wajisajili kabla ya siku ya mkutano. Watanzania takriban 200 walijisajili na
ubalozi ulifanya maandalizi ya ukumbi, vyakula na vinywaji kwa ajili ya watu
300 kwenye hoteli ya Golden Tulip.
Siku
ya mkutano ilipowadia, Watanzania zaidi ya elfu moja walijitokeza na
kusababisha ugumu wa kuendelea na mkutano kutokana na maandalizi yaliyofanywa
yalilenga watu 300.
Kamati
ya maandalizi ilipoona ukumbi umejaa na watu walio nje ni weng mara mbili zaidi
ya watu waliokuwemo ndani ya ukumbi iliamua kufunga milango na kuwaomba
waliochelewa warejee nyumbani.
Uamuzi
huo haukuwafurahisha watu waliochelewa, hivyo walishinikiza waingizwe kwenye
ukumbi wa mkutano, kitendo ambacho kiliashiria uwezekano wa kutokea vurugu
kubwa.
Kutokana
na uhalisia huo, Kamati ya maandalizi ambayo ilijumuisha pia viongozi wa
Watanzania wanaoishi nchini humo ilishauriana na kuamua kuwa mkutano huo uahirishwe
na maandalizi yaanze upya kwa madhumuni ya kupata ukumbi na huduma nyingine
zitakazokidhi idadi kubwa ya watu.
Kutokana
na ufafanuzi huo, Wizara inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa kipande
hicho cha video kimechukuliwa wakati Watanzania wanashinikiza kuingia kwenye
ukumbi wa mkutano na sio kwamba wamekusanyika kwenye ofisi ya ubalozi wa
Tanzania kushinikiza kurejeshwa nyumbani kutokana na mateso wanayoyapata.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 26 Machi,
2018
No comments:
Post a Comment