Advertisements

Friday, March 2, 2018

Wanafunzi wa Udom waunga mkono Jitihada za Elimu Bure

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo (aliyesimama) akitoa hotuba yake kabla ya kuzindua programu ya wanafunzi walimu kutoka Chuo Kikuu cHa Dodoma wanaokwenda kujitolea kwenye shule za Sekondari na Msingi zilizo karibu na maeneo wanayoishi.
 Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma, Pro.Davis Mwamfupe akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kuzindua program ya wanafunzi walimu wa UDOM wanaokwenda kujitolea kwenye Shule za Msingi na Sekondari.
 Mratibu wa program ya kujitolea kwa Wanafunzi Walimu Dr. Ombeni Msuya ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma akielelezea namna walivyojipanga kusimamia program hiyo.
 Mwenyekiti wa Wanafunzi Walimu wanaokwenda kujitolea akizungumza kwenye uzinduzi wa Programu hiyo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Shule ya Sekondari Umonga iliyopo Mjini Dodoma.
Baadhi ya wanafunzi walimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi kabla ya uzinduzi wa program maalumu ya kwenda kujitolea kwenye Shule za msingi na sekondari.

Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma wanaosomea Shahada ya Ualimu wameunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika  Utoaji wa Elimu Msingi bila malipo kwa kujitolea kwenda kufundisha katika shule za msingi na Sekondari zilizoko katika maeneo yao wakati wa Likizo.

Akizindua mpango huo wa kujitolea kwa wanafunzi walimu zaidi ya 500 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo amewataka wanafunzi hao kuwa mfano ya kuigwa kwenye shule watakazoenda kufundisha ili kuipa heshima zaidi programu hii iweze kuwavutia walimu wengine zaidi.

Alisema kuwa mnapofika mashuleni mkawe mfano bora kwa wadogo zenu, mkaonyeshe uwezo wenu katika kufundisha na kuwafikishia yale muhimu katika masomo yao, mkaonyeshe Umahiri katika Taaluma yenu ndipo kujitoa kwenu kutaheshimiwa na kuthaminiwa na jamii nzima ya watanzania.

Aliongeza kuwa wanafunzi wa UDOM mnaokwenda kujitolea ndio mtakua waasisi wa programu hii kitaifa hakuna eneo lolote Nchini ambako wanafunzi walimu kwa Umoja wao waliamua kwa hiari kwenda kufanya kazi katika jamii walizotoka tena bila malipo yeyote kwa wengine watakaofanya hivi katika maeneo yao watakua wameiga kutoka kwenu.

“Huu ni Uzalendo wa hali ya juu na mmejitoa kwa Taifa lenu na kupitia kujitolea kwenu mnasaidia kutatua changamoto zinazokabili Wizara ya TAMISEMI hakika mnapaswa kutambuliwa na kuweka kumbukumbu sahihi ya nani na nani alishiriki katika program hii” Alisema Jafo.

Akizungumza katika Uzinduzi wa kampeni hiyo Meya wa Manispaa ya Dodoma Mhe.Prof.Davis Mwanfupe amewaasa wanafunzi walimu wanaokwenda kujitolea na kuwakumbusha kwenda kuitumia vyema Taaluma yao kwa kuwa Nuru ya kuiangazia jamii katika mambo yale yaliyo mema.

Naye Mratibu wa Programu hii ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma Dr.Ombeni Msuya amesema huu ni muendelezo wa kampeni ya Nipe Daftari na Peni, Nami nipate Elimu iliyozinduliwa na Waziri Jafo hivi karibuni.

Amesema sababu ya programu hii inatokana na ukweli kwamba shule nyingi za Serikali zina Upungufu wa Walimu kutokana na Upatikanaji wa Elimu bure ambao umeongeza Idadi ya wanafunzi katika shule nyingi kuanzia Msingi hadi Sekondari hivyo wakaona ni vyema kuratibu wanafunzi walimu waweze kwenda kuunga Mkono jitihada hizi za Serikali.


Hata hivyo Dr. Abdallah Seni ambaye pia ni miongoni mwa waratibu wa Programu hii alisema sisi ni sehemu ya wanataaluma na wataalamu, kwa pamoja tumeazimia kuhamasisha walimu wanafunzi na walimu wengine wanaofanya kazi nje ya Ualimu, kuitikia wito wa kujitolea kufundisha katika shule ambazo wapo jirani nazo kama sehemu ya uzalendo na upendo kwa Nchi yao.

No comments: